Na Dotto Kwilasa,DODOMA
MENEJA Shirika la Viwango (TBS)Kanda ya kati Nickonia Mwambuka amewataka wananchi kutumia maonesho ya wakulima-Nanenane kujifunza uzalishaji wa bidhaa zenye ubora na kuleta usalama kwa Afya ya jamii.
Amesema ,wao wakiwa na dhamana ya ubora,wana wajibu wa kuelimisha Umma juu ya masuala yote yanayohusu uwekaji na usimamizi wa viwango pamoja na udhibiti wa ubora wa bidhaa viwandani.
Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini hapa mara baada ya kutembelewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida Dkt. Paskas Mragiri katika banda hilo kwenye viwanja vya maonesho vilivyopo Nzuguni, Meneja huyo amesema hali hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na bidhaa zisizo na ubora kwenye soko.
Mbali na hayo ameshauri walaji kuwa na mazoea ya kutumia bidhaa zenye alama ya ubora wa TBS ambaoo bidhaa husika huonesha kuwa imepimwa na kuthibitishwa ubora wake na kueleza kuwa alama hiyo ni uthibitisho kwa mzalishaji na mlaji kuwa bidhaa husika ni bora na salama kwa matumizi na Mazingira.
Amesema alama ya ubora ya TBS huwafanya wanunuzi kununua bidhaa na kutumia bila wasiwasi wowote.
"Alama hiyo humlinda mzalishaji katika ushindani dhidi ya bidhaa hafifu na kumuwezesha kulihakikishia soko lake kuwa bidhaa yake inakidhi matakwa yaliyobainiswa matika kiwango na hivyo ni bora na Salama kwa matumizi yaliyokusudiwa," amesema Meneja huyo
Pamoja na hayo amesema "TBS ina skimu mbili za udhibiti ubora mojawapo ya skimu hizo ni Skimu ya alama ya ubora ambapo chini ya skimu hii mzalishaji ambaye bidhaa yake imethibitishwa ubora kwa kuzingatia kiwango cha kitaifa cha bidhaa husika hupewa leseni ya kutumia alama ya TBS Katika bidhaa hiyo,"alisema Mwambuka .
Hata hivyo alipoulizwa na Mkuu wa Wilaya ya Singida Paskas Mragiri juu ya bidhaa bandia zinazosafirishwa kutoka Mikoa na nchi mbalimbali Meneja huyo amesema wamekuwa wakifanya kaguzi za mara kwa mara na wamekuwa wakikamata na kutelekeza bidhaa hizo bandia.
Hata hivyo Shirika limetenga TZS 581 Milioni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uthibitishaji wa mifumo ya kiutendaji ambapo kwa sasa TBS imepatiwa ithibati ya kufanya shughuli hiyo na mashirika yanaweza kuthibitishiwa ubora wa mifumo yao ya kiutendaji kupitia TBS hiyoitasaidia kuhakikisha wananchi wanapokea huduma zilizo bora.
Pamoja na hayo Meneja huyo ameeleza majukumu ya shirika hilo kuwa ni pamoja na kutoa ushauri viwandani juu ya uzalishaji wa bidhaa bora,kupima na kuhakikisha vpimo vinavyotumika viwandani na kudhibiti wa bidhaa zenye ubora hafifu.