Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko
**
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amewasihi wakuu wa kaya kuhakikisha wanaacha taarifa muhimu wanapoondoka nyumbani, ili kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na makazi linaloendelea nchini kote.
Mboneko amezitaja taarifa hizo kuwa ni pamoja na Namba za kitambulisho cha taifa (NIDA), kwa kila mwanafamilia mwenye sifa ya kuwa na kitambulisho hicho, kadi ya Bima ya Afya kwa wenye nazo, pamoja na namba za simu za mkuu wa Kaya.
Amesema namba hizo ni muhimu kuachwa kwa anayebaki nyumbani, ili makarani wa Sensa wazitumie kumpigia mkuu wa Kaya pale wanapohitaji ufafanuzi wa taarifa mbalimbali.
Wakati huohuo Mboneko amewasisitiza Wananchi kuendelea kushirikiana na Makarani wa Sensa, pale wanapofika katika familia zao, ili kufanikisha zoezi hilo, ambalo ni muhimu katika kuiwezesha Serikali kupanga mipango ya Maendeleo.
Zoezi hilo la Sensa ya Watu na makazi ambalo limeanza nchini kote Jumanne Agosti 23 ,2022, limeelezwa kuwa litachukua muda wa siku kumi mpaka kukamilika kwake, ambapo kwa muda wa siku sita kuanzia siku ya kwanza ya Agosti 23 hadi Agosti 28, 2022, Makarani Sensa watajielekeza katika kuchukua taarifa za Wanafamilia pekee, ambapo siku nne zilizosalia kuanzia Agosti 29 hadi 31 mwaka 2022, watarudi tena kwenye kaya walizopita kwa ajili ya kuchukua taarifa za Majengo.
Zoezi hilo ambalo kwa mwaka huu linafanyika Kidigitali, linachukua muda wa siku kumi kutokana na taarifa muhimu zinazohitajika, ambazo hazikuwemo kwenye Madodoso ya Sensa zilizopita.
Social Plugin