Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ULEVI CHANZO CHA ONGEZEKO LA UKATILI WA KIJINSIA KATA YA VUMARI


Wananchi wa Kata ya Vumari iliyopo Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, wametaja ulevi uliokithiri wa pombe za kienyeji kama chanzo kikuu cha ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji na ulawiti.


Wakizungumza katika kikao kilichojumuisha viongozi wa Kata, na waraghibishi wa Kata hiyo, wanasema matukio ya ukatili wa kijinsia yamekuwa na athari kwenye jamii hiyo ikiwemo kuvunjika kwa familia,kusababisha mmomonyoko wa maadili pamoja na kurudisha nyumba maendeleo ya eneo hilo.


Wananchi wa Kata ya Vumari wameweza kuibua changamoto zilizopo kwenye eneo lao pamoja na njia za kuzitatua baada ya kupatiwa mafunzo na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),yaliyowajengea uelewa katika masuala ya jinsia, ukatili wa kijinsia, uongozi, pamoja na huduma za kijamii na maendeleo kwa ujumla.


William John mkazi wa Kijiji cha Vumari, akisoma risala mbele ya viongozi wa kata hiyo anasema eneo hilo lina matukio mengi ya ukatili wa kijinsia ikiwemo, lugha za udhailishaji wa kingono, ukatili wa kisaikolojia, ukatili wa kiuchumi, ulawiti, na ubakaji,ambao unasababishwa na ulevi, uvutaji bangi,ulaji wa mirungi, pamoja na mila na desturi kandamizi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Vumari Bakari Said anasema pombe nyingi zinazosababisha ulevi kwa jamii hiyo ni zile za kienyeji ikiwemo gongo,uvutaji wa bangi pamoja na ulaji wa mirungi ambazo zimekwishapigiwa kelele kwa muda mrefu bila mafanikio, ambazo zimesababisha mmonyoko wa maadili kwa vijana kwa kiwango kikubwa.

“Vijana wengi ambao ni wanyaji wa hizi pombe wametelekeza familia,na kuachia jukumu la kulea familia wanawake, ndiyo maana eneo letu tunatatizo kubwa la njaa kwa sababu wanaume wengi hawashiriki shughuli za uzalishaji wanawaachia wanawake”,anasema Stella John Mraghbishi kata Vumari.


Akiuzumza katika kikao hicho Diwani wa Kata ya Vumari, John Msofe anasema tatizo la unywaji wa pombe ni kubwa kwenye kata hiyo ambalo ni tatizo la muda mrefu,ambalo limekuwa na madhara mengi ikiwemo kusababisha vifo kwa wananchi.


Msofe anasema ili kumaliza tatizo la ulevi inahitajika nguvu ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi kwani kwa muda mrefu ambao wamekuwa wakiripoti za ulevi na utengenezaji wa pombe hakuna hatua hatua zilizochukuwa mpaka sasa.


Changamoto nyingine zilizowasilishwa na waraghibishi wa kata hiyo mara baada ya kushiriki utafiti uliofanywa na shirika la TGNP, chini ya mradi wa Wanawake wa vijijini kuchechemua mabadiliko, wanasema pia katika eneo hilo wanakabiliwa na changamoto katika sekta ya afya,elimu,miundombinu Pamoja na migogoro baiana ya wakulima na wafugaji ambazo zote zinahutaji kutafutiwa ufumbuzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com