Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Ally Makame Hamad
Na Walter Mguluchuma - Katavi
JESHI LA POLISI Mkoa wa Katavi limemkamata na linamshikilia Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Mpimbwe Mkoani Katavi Dickson Beno Mwenda (37) kwa tuhuma za kumbaka msichana (15) ndani ya gari aina ya Noah baada ya kukabidhiwa na mama mzazi wa mtoto huyo amfikishe nyumbani kwao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Ally Makame Hamad amewaambia waandishi wa vyombo mbambali kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Agosti 13,2022 majira ya saa moja na nusu usiku katika eneo la Kijiji cha Kibaoni Tarafa ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele.
Amesema kuwa siku ya tukio hilo mama mzazi wa msichana huyo walikuwa Baa na mtuhumiwa Dickson Mwenda wakinywa vinywaji pamoja na msichana huyo.
"Baada ya kuwa wamekunywa pombe kwa muda mrefu mtuhumiwa aliona ametosheka na ndipo alipomuaga mama wa mtoto huyo kuwa anataka kurejea nyumbani kwake alikokuwa akiishi kwenye Kijiji cha Usevya yalipo makao ya Halmashauri ya Mpimbwe.
"Ndipo mama wa mtoto huyo ambaye yeye alikuwa bado anaendelea kupata kinywaji alimuomba mtuhumiwa amsaidie kumpeleka nyumbani msichana huyo aliyekuwa na mdogo wake kwa lengo la kuwapeka nyumbani",ameeleza.
Kamanda Hamad ameeleza kuwa baada ya kukabidhiwa watoto hapo ndipo alipowapakiza kwenye gari lenye Namba za usajili T,927 DMC aina ya Toyota Noah kwa ajili ya kuwapeleka nyumbani kwao katika Kijiji cha Usevya.
"Wakati wakiwa wanaendelea na safari hiyo wakiwa njiani mtuhumiwa Dickson aliegesha gari pembeni mwa barabara na kisha alianza kutekeleza unyama huo humo humo ndani ya gari hilo mpaka alipomaliza haja zake",amesimulia.
Alisema baada ya kufanyika kwa tukio hilo binti huyo alitoa taarifa kwa mama yake ambaye naye aliripoti katika kituo cha polisi na polisi baada ya kupata taarifa hizo walimsaka mtuhumiwa na kumkamata.
Kamanda huyo wa polisi amesema upelelezi wa tukio hilo umekamilika na mtuhumiwa ambaye bado anashikiliwa na jeshi hilo anatarajiwa kufikishwa Mahakamani wakati wowote wiki hii.
Social Plugin