Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KITABU KIPYA CHA WATOTO 'THE AFRICAN ALPHABET' CHAZINDULIWA DAR ES SALAAM


Baadhi ya watoto waliohudhuria walipata fursa ya kupiga picha na mtunzi wa kitabu Kemilembe Mugangala na Mgeni Rasmi Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Bonaventure Rutinwa Profesa Bonaventure Rutinwa
***

-Mwandishi wake asema usomaji vitabu unaongeza ubunifu, maarifa na uelewa kwa watoto

Kitabu kipya cha Watoto kinachojulikana kama - The African Alphabet - kimezinduliwa leo jijini Dar es Salaam na kinapatikana kwenye maduka ya kuuza vitabu na ,na kwenye mtandao wa kuuza machapisho wa kimataifa wa Amazon.

Mwandishi wa kitabu hiki ni Kemilembe Mugangala, ambaye ni Mwanafunzi wa mwaka wa nne katika Chuo Kikuu cha Drake nchini Marekani, anayesomea fani ya utengenezaji wa vipindi kwa mfumo wa kidigitali (digital media production) ,kimelenga kufundisha watoto wa madarasa ya awali herufi kwa kutumia alama na majina yanayoendana na mazingira ya Kiafrika.

Akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi, Mugangala alisema kilichomsukuma kuandika kitabu hiki ni uzoefu wa mazingira aliyosomea kuona watoto wanajifunza kwa kutumia vitabu vilivyoandikwa kwa utamaduni na mazingira ya nchi za Magharibi wakati Tanzania na Afrika kwa ujumla tuna tamaduni zetu, ambazo ni rahisi kutumika na watoto kuelewa zaidi.

 Alitoa mfano kuwa watoto wanaweza kufundishwa kwa kutumia herufi A ni Afrika, M ni kwa Matoke,Z ni kwa Zanzibar na maneno mengine mengi yaliyopo kwenye maeneo yaliyowazunguka.

Alisema utumiaji wa maneno ya Kiafrika kwa watoto wakati wa kujifunza herufi na maneno kunarahisisha kupata uelewa wa mila na tamaduni zao na mazingira wanayoishi.Hatua hii inawajengea msingi wa kuwa wabunifu katika kutatua na kupambana na mazingira yaliyowazunguka katika jamii wanazoishi.

“Kama mnavyojua elimu ya awali ndiyo msingi wa kumjenga mtoto katika safari yake ya elimu, hivyo hatua hii ni muhimu sana watoto kupata vitabu vya kusoma vilivyoandikwa kwa lugha nyepesi kueleweka kwao, ambavyo vinaweza kuwajengea uwezo wa kujua masuala mbalimbali na kujitambua, mila na utamaduni wao ,alisema Muganga wakati wa hafla ya uzinduzi ambapo Mgeni Rasmi alikuwa ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Profesa Bonaventure Rutinwa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta ya elimu na watoto wa shule za chekechea", alisema.

Mugangala, ambaye alisomea katika Shule za Kimataifa nchini Tanzania na nje ya nchi alisema japo elimu yenye mwelekeo wa nchi za Magharibi ni bora lakini mitala yake haiwalengi watoto wa Kiafrika kuthamini mila na tamaduni zake.

Alisema kitabu cha The African Alphabet kinahamasisha uthamini wa mila za Kiafrika hususani katika kipindi hiki cha utandawazi ambapo wazazi wengi hawapati muda wa kutosha wa kukaa na watoto wao hali inayosababisha watoto kujifunza mila,imani na tamaduni za kigeni.

Alieleza zaidi kuwa kadri dunia inavyoingia kwenye utandawazi,mila na tamaduni na Tanzania na Afrika kwa ujumla zinazidi kupotea kiasi kwamba katika siku za usoni tutakuwa na kizazi kisichojua mila na tamaduni zetu kwa kuwa Waafrika tumebaki nyuma katika kufundisha vijana mila zetu kwendana na mtandao wa kidunia ambapo dunia imeunganishwa na matumizi ya teknolojia za kisasa.

“Kutokana na maendeleo ya teknolojia ya sayansi na TEHAMA, kumekuwepo na mabadiliko ya tamaduni mbalimbali kutokana na matumizi ya internet na vifaa vya kisasa vya kieletronic kama simu janja (smart Phones), Kompyuta ,luninga na mitandao ya kijamii nk. Hivi vyote vimeendelea kuleta athari katika jamii zetu kwa kuwa mambo mengi mazuri ya mila na tamaduni zetu hayapatikani kwenye teknolojia hizo hivyo watoto wa kitanzania na kiafrika kwa ujumla wanaishia kulishwa maudhui (contents) zenye mwelekeo wa kigeni na kusoma vitabu na kuangalia vikaragosi (Cartoons) kwenye luninga zenye mwelekeo wa kimagharibi. Siku hizi ni jambo la kawaida kukuta watoto Wadogo wengi wakitumia muda wao mwingi kuangalia luninga, kuchezea Simu janja (Smart phones na laptop, ”alisema.

Alitoa wito kwa wadau wote wa tasnia ya uandishi wa vitabu kushirikiana pamoja, kuzidi kutunga vitabu vizuri vya kusisimua ili kufufua ari na mwamko wa Watanzania kupenda kusoma na sio kusoma tu bali kusoma vitabu vyenye kuwajengea uwezo wa kupata maarifa.

Aliiomba Serikali kupitia Wizara elimu na taasisi nyinginezo zinazosimamia elimu, iangalie jinsi ya kusaidia tasnia ya uandishi na uchapishaji vitabu pia ikiwezekana waandishi wa vitabu vyenye mwelekeo wa kusaidia jamii zetu wapatiwe ruzuku ya kuwawezesha kufanikisha kazi zao, sambamba na vitabu vyao kuidhinishwa kutumika mashuleni.

 Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Bonaventure Rutinwa, alimpongeza Mugangala, kwa kutunga kitabu hicho kwa lugha nyepesi inayoweza kueleweka kwa watoto sambamba na kuzingatia kuwezesha watoto kuelewa utamaduni na mazingira ya Kitanzania na Kiafrika.

Alisema sekta ya usomaji vitabu ni muhimu katika kujenga kizazi cha jamii yenye maarifa hivyo alitoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanawapatia vitabu vya kusoma ili wapate maarifa.Alisema kutokana na mabadiliko makubwa ya TEHAMA kuna umuhimu mkubwa wa kupambana kulinda mila na utamaduni wetu wa Kiafrika usipotee.
Mgeni Rasmi Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Profesa Bonaventure Rutinwa, akiongea na wageni waalikwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu cha watoto cha The African Alphabet.
Mtunzi wa kitabu cha watoto cha The African Alphabet ,Kemilembe Mugangala akiongea wakati wa hafla ya uzinduzi.
Mgeni Rasmi  Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Profesa Bonaventure Rutinwa (kulia) akionesha nakala ya kitabu cha The African Alphabet wakati wa hafla hiyo (Kushoto) ni mtunzi wa kitabu hicho Kemilembe Mugangala.
Mgeni Rasmi Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Profesa Bonaventure Rutinwa na mtunzi wa kitabu cha The African Alphabet walijumuika na watoto waliohudhuria hafla hiyo kuwafundisha jinsi ya kukisoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com