Tume Huru ya uchaguzi ya Kenya (IEBC) imemtangaza William Ruto kuwa Rais Mteule wa Kenya kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo. Ruto alikuwa anachuana vikali na Raila Odinga.
Mgombea wa Urais kupitia Chama cha UDA nchini Kenya William Ruto ndiye Rais mteule nchini humo.
Ruto ameibuka mshindi baada ya kumshinda mpinzani wake wa karibu Raila Amollo Odinga wa Muungano wa Azimio baada ya kupata kura 7,176,141 dhidi ya mpinzani wake mkuu aliyepata 6,942930.
Akitangaza matokeo hayo katika ukumbi wa Bomas , mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chebukati amesema kwamba Ruto amejipatia asilimia 50.49 ya kura naye Raila akaijipatia asilimia 48.85.
Vilevile mgombea wa chama cha Roots Party George Wajackoyah alipata 69969 huku mwenzake wa chama cha Agano Waihiga Mwaure akijipatia 31987.
Ruto ametangazwa mshindi huku kukiwa na mgawanyiko baada ya mgombea wa Muungano wa Azimio Raila odinga kususia sherehe ya kumtangaza mshindi.
Makamishna wanne wa tume hiyo walizungumza na waandishi wa habari wakidai kwamba hawataki kuhusishwa na matokeo hayo kutokana na jinsi shughuli ya uchaguzi ilivyoendeshwa.
Akizungumnza katika hotuba yake punde baada ya kutangazwa mshindi , Bwana Ruto alisema kwamba angependa kumshukuru Mungu kwa kumfikisha katika hatua hii.
''Najua kwamba baadhi ya watu walibashiri kwamba hatutafika hapa lakini kwa sababu kuna Mungu Mbinguni tumefika. Shukran zangu ziwaendee Wakenya wote''.
Awali akimtangaza mshindi Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi IEBC Wafula Chebukati alisema: Tumetembea safari ya kuhakikisha kwamba Wakenya wanashiriki katika uchaguzi ulio huru na wa haki.
Ruto aipongeza tume ya uchaguzi
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa Urais , rais Mteule William Ruto amepongeza shughuli nzima ya uchaguzi , licha ya kwamba baadhi ya makamishna hawakuweza kushiriki katika matangazo rasmi
WILLIAM RUTO NI NANI??
William Ruto, ni miongoni mwa wanasiasa wengi wakubwa nchini Kenya walioweka wazi nia zao za kuingia Ikulu ya Kenya, kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, kurithi mikoba ya aliyekuwa 'swahiba wake', Uhuru Kenyatta.
Mwanasiasa huyu tajiri ambaye amekuwa na ndoto za kuwa Rais wa Kenya, amekuwa akikutana na vikwazo lukuki vya kisiasa, ikiwemo kuzuiwa kwa sababu ama kuzuiwa kwa makusudi kufanya shughuli kadhaa za kisiasa na binafsi kutokana na msukumo wa kisiasa.
Ni miongoni mwa wanasiasa mashuhuri nchini humo, walioweka wazi nia zao za kuingia Ikulu ya Kenya, kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, kurithi mikoba ya 'swahiba wake', Uhuru Kenyatta.
Lakini Ruto ni nani hasa?
Ruto anatoka katika familia ya kawaida tu na kuwa mwanasiasa tajika nchini Kenya. Anatokea kwenye jamii ya Wakalenjin alizaliwa Disemba 21, 1966 katika kijiji cha Sugoi, magharibi mwa Rift Valley.
Elimu yake ya msingi na sekondari amesomea katika shule za kawaida kabla ya kujiunga na Chuo kikuu cha Nairobi. Waliosoma naye hasa shule ya sekondari wanamkumbuka Ruto kama 'mtu mtaratibu, mwenye haya na wakati wote akijiweka kama mtu wa kawaida tu".
Ruto (katikati), amekuwa hafichi nia yake ya kuingia Ikulu ya Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2022
Kwa mujibu wa mama yake, Sara Cheruiyot, "hakuwa mkaidi" na wakati wote alikuwa 'mtiifu, mwaminifu na anayefika kwa wakati'. Hakuwa mtu anayependa ugomvi ama kugombana na wenzake, muda mwingi alikuwa akibeba kitabu kwa ajili ya kujisomea.
Akiwa chuo Kikuu, alikuwa kiongozi wa kwaya ya umoja wa wakristo chuoni hapo. Akiwa kwenye masuala hayo ya kwaya ya kanisa, alikutana na mtu aliyemuhusudu sana kwenye siasa, rais wa zamani wa nchi hiyo, Daniel arap Moi. Kama ilivyo kwa Ruto, Rais Moi pia anatokea kenye jamii ya Wakalenjini na muumini wa kanisa.
Ruto alisaidia kuanzishwa kwa kikundi cha vijana kilichoitwa Youth for Kanu 92 (YK92), ambacho Moi alikitumia kurejea madarakani mwaka 1992. Moja ya kampeni kubwa ya kikundi hicho ilikuwa ni kumwaga mabilioni ya pesa, hatua ambayo baadae ilikuja kulaumiwa kuwa chanzo cha mtikitiso wa uchumi katika miaka ya mwanzoni mwa 1990s. Inaeleweka kwamba wakati huu, ndio Ruto alipotengeneza utajiri wake.
Siasa zake hazitofautiana na wanasiasa wengi wa Kenya
Ruto aliingia kwenye siasa kwa mgongo wa kundi la vijana la Youth for Kanu 92 (YK92). Alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 1997 na muda mfupi baadae akawa mmoja wa wanasiasa wakubwa nchini Kenya.
Wakati KANU ilipoanguka mwaka 2002, Moi alimteua Ruto kuwa naibu waziri wa mambo ya ndani, kabla ya kumpandisha cheo na kuwa waziri kamili. Mpaka wakati huo maafisa wengi wakubwa walijiondoa katika chama tawala hasa baada ya kuteuliwa kwa Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wa kiti cha Urais na kupewa Baraka na Moi.
Ingawa KANU ilishindwa uchaguzi, Ruto alitetea kiti chake cha Ubunge na akachaguliwa kuwa katibu mkuu wa chama hicho mwaka 2005. Ilipofika mwaka 2006 akatangaza nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Rais Kenyatta (kushoto) na naibu wake Ruto (kulia) walikuwa wakiitwa mapacha, kutokana na 'uswahiba wao kwenye chaguzi zilizopita kupitia Jubilee
Akaanza kufanya kazi kwa karibu na Raila Odinga, waziri wa zamani na hasimu mkubwa wa Rais Moi. Alitumia sana Radio maarufu kwa Wakalenjini, Kass FM, kama jukwaa la kupitishia ajenda zake.
Alihama chama cha KANU na kujiunga na chama cha Odinga cha Orange Democratic Movement (ODM). Kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kutafuta fursa nzuri ya kisiasa ni siasa zilizoshamiri sana Kenya kwa sasa, na wanasiasa wengi wamekuwa wakifanya hivyo, jambo ambalo halimtofautishi na wanasiasa wengine.
Ruto alishindwa katika kura za ndani za kumsaka mgombea urais kupitia ODM, lakini alikuwa mstari wa mbele kushawishi mamilioni ya wananchi wa eneo bonde la Ufa anakotokea na maeneo mengine kumuunga mkono Raila Odinga, kiasi cha hata kura za maoni kuonyesha kwamba alikuwa anashinda uchaguzi mkuu wa 2007.
Alikuwa mtu wa karibu wa Odinga na mpiganaji wake wakati wote wa uchaguzi na zoezi la kuhesabu kura. Mamlaka za uchaguzi zikamtangaza Rais Mwai Kibaki kumshinda Odinga na hapo ukawa mwanzo wa ghasia kubwa za kikabila zilizodumu mwaka hadi Februari 2008, Kibaki na Odinga walipokubaliana kuunda serikali ya Muungano. Ruto akateuliwa kuwa waziri wa kilimo.
Ruto (kushoto) na Odinga (kulia), walikuwa 'maswahiba'
Kama sehemu ya makubaliano, uchanguzi wa vurugu hizo ukafanyika, na wote Rais Kibaki, waziri mkuu Odinga wakaishia kwenye tuhuma za ndani, huku Ruto ambaye tayari walishatofautiana na Odinga, akapelekwa kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC).
Ruto alikana kwa nguvu tuhuma zozote za kuhusika kwake na ghasi na kusema anachokiamini ni kwamba, tuhuma hizo ni za kutungwa.
Novemba 2012, aliungana na Kenyatta kuunda Jubilee Alliance. Kupitia muungano huo, walitumia kesi yao huko ICC kujijenga kisiasa na kueleza mashataka dhidi yao ni kuingilia uhuru wa Kenya. Mkakati wao ulifanya kazi na kuendelea kuwa Rais na makamu wake mpaka sasa
Ruto na Misukosuko yake ya kisiasa
Kuwa mwanasiasa kunahitaji uwe na ngozi ngumu, lakini kuwa sehemu ya Ruto kunahitaji kuwa ngozi ngumu zaidi, ni miongoni mwa wanasiasa wachache waliopitia masahibu makubwa katika maisha yao ya siasa Kenya.
Amekuwa akizongwa na vitendo vya rushwa ambavyo mara zote amekuwa akikana kuhusika navyo. Mwezi Februari 2009, almanusura apigiwe kura za kutokuwa na Imani naye kutokana na kashfa ya mahindi chini ya wizara yake.
Oktoba 2010 akawekwa kando kwenye baraza la mawaziri kufuatia tuhuma za kuuza ardhi ya umma. Baadae akarejeshwa. Juni 2013, mahakama kuu ilimuamuru kusalimisha heka 100 na kumpa fidia mkulima ambaye alimtuhumu Ruto kumpokonyaa ardhi hiyo wakati wa vurugu za mwaka 2007.
Hata hivyo amekuwa akisisitiza kwamba yeye hana shida, hana tatizo, na kusema utajiri wake unatokana na juhudi zake za kuchapa kazi.
"Niliuza kuku katika maeneo ambayo reli inakatiza karibu na nyumbani kwetu, nikamjengea baba yangu nyumba kwa kutumia mkopo wangu wa chuo, nikawalipia ada ndugu zangu. Mungu amekuwa mwema kwenye juhudi zangu, nashukuru nimejaliwa," aliiambia gazeti la The Star nchini Kenya.
Kasheshe lingine kubwa ambalo hawezi kulisahau Ruto ni la kufikishwa katika mahakama ya ICC. Aliyewasilisha majina ya waliohusika kwenye ghasia za Kenya, alikuwa Kofi Annan msuluhishi na aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Ruto aliwahi kuliambia gazeti la Sunday Nation la Kenya mwaka 2009 kwamba, Annan "anapaswa kuwasilisha bahasha hiyo… ili uchunguzi mzuri uweze kuanza."
Mahakama hiyo iliondoa mashtaka kwa washukiwa wengine na kusalia na Kenyatta, Ruto na Joshua arap Sang, mwandishi kutoka redio Kass FM radio ambaye alituhumiwa kwa kuchochea vurugu kwa kusaidia kuratibu mashambulizi dhidi ya jamii ya wakikuyu.
Mbali na hayo, Ruto amezuiwa mara kadhaa kufanya mikutano ya kisiasa na hivi majuzi amezuiwa kusafiri kwenda Uganda , kwa shughuli binafsi kukutana na Rais Yoweri Museven.
Kupeana mikono kwa Uhuru na Odinga, kulikotingisha uhusiano wake na Uhuru
Hatua ya Rais Kenyatta (kushoto) na aliyekuwa hasimu wake Odinga (Kulia) kupeana mikono, kumekuwa mwanzo wa mtikisiko wa siasa za Ruto kwenye Ikulu
Uhusiani wa Ruto na Kenyatta, kwa mara ya kwanza ulianza kutikisika mwezi machi 2018, wakati Rais Uhuru Kenyatta, alipomtambulisha na kumkaribisha hasimu wake wa zamani Odinga kama mshirika wake mwingine wa tatu.
Baada ya uchaguzi wa mwaka 2017 Odinga, ambaye alikuwa sehemu ya muungano mwingine wa NASA, akiwa na washirika wengine, alipinga matokeo ya uchaguzi huo akisema hayakuwa sahihi kwa vile uchaguzi haukuwa huru nawa haki.
Uhuru akatumia nafasi yake ya Urais kumleta karibu zaidi Odinga wakati huu anakwenda kumaliza muhula wake wa pili wa urais, na kupeana mikono kuashiria kumalizika kwa uhasama wao kisiasa na kusisitiza Amani iliyoanza kutetereka baada ya matokeo ya uchaguzi.
Kenyatta hakutaka kurejea kwenye ghasia za mwaka 2007 zilizoua maelfu ya Wakenya. Alitaka Amani, na Amani hiyo aliona inawezekana kama atamsogeza karibu Odinga.
Taaratibu, Ruto akawa anawekwa mbali huku Odinga akisogezwa karibu. Kwa sasa uhusiano wao wa mashaka umekuwa wazi zaidi. Namna wanavyozungumza, namna wanavyoshughulikia masuala yao na namna wanavyoshirikiana, inakuonyesha uhusiano wao hauko kama wa zamani, na hilo linaleta picha ya uchaguzi ujao utakavyokuwa.
Pamoja na kuonekana wazi, kwenda tofauti na Uhuru, Ruto amegoma kuachia ngazi nafasi yake ya naibu Rais, kama inavyoshauriwa na wengi. Lakini wadadisi wanasema kusalia kwakwe kwenye nafasi hiyo kunampa nguvu na jukwaa la kuendelea na harakati zake za kuingia Ikulu mwakani.
Huenda Odinga akaungwa mkono kwa uwazi na Uhuru kwenye uchaguzi mkuu ujao, na kumuacha 'swahiba' wake Ruto aliyejipanga kwa muda mrefu kuwania urais.
CHANZO - BBC SWAHILI
Social Plugin