Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TEA YASAIDIA VYUMBA VYA MADARASA CHALINZE

Afisa Elimu ya msingi wa halmashauri ya Chalinze Bi. Miriam Kihiyo akihutubia Wananchi katika viwanja vya shule ya msingi Kibiki
**

NA. ELISANTE KINDULU, CHALINZE

MAMLAKA ya Elimu Tanzania (Tanzania Education Authority-TEA), imeendelea kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo ,mkoa wa Pwani.


Akizungumza na Wananchi katika mkutano maalumu wa wazazi na wadau wa Elimu katika viwanja vya shule ya msingi Kibiki, afisa Elimu ya msingi wa halmashauri hiyo Bi. Miriam Kihiyo alisema kwamba, shule 37 ziliomba hisani ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kutoka kwa wafadhiri hao lakini uwezo uliruhusu vyumba vitatu tu.


Bi. Miriam ameipongeza mamlaka hiyo ya Elimu kwa kuendelea kuiona Chalinze kwa jicho la pekee, ambapo mwaka 2021, TEA waliwezesha ujenzi wa madarasa 4 katika mji wa Chalinze, vikiwemo vyumba 2 katika shule ya msingi Chalinze na vyumba 2 katika shule ya msingi Bwilingu "B".


Afisa Elimu huyo msingi aliieleza hadhira hiyo kuwa katika chumba kimoja Cha darasa kimetolewa shilingi milioni 20 ambazo bado zitahitajika nguvu ya Wananchi kukamikisha ujenzi huo kwa darasa moja.


Afisa Elimu aliishukuru pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia bweni la watoto wenye mahitaji maalumu pamoja na madarasa 14 ya shule shikizi za msingi zilizotoka na mradi wa UVIKO -19 mwaka jana.


Naye Diwani wa kata ya Bwilingu Nasser Kalama amewaomba wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania hususani kwenye sekta ya Elimu.


"Mwaka Jana hapa Kibiki tulipata mradi wa ujenzi wa vyoo vya shule. Na mwaka huu tumepata mradi wa kisima na vyumba vitatu vya madarasa. Niwaombe ndugu zangu kunapotokea Jambo la kusaidia nguvu kazi katika ujenzi wa madarasa hayo tujitokeze bila kinyongo", alisema Diwani Nasser.


Akimkaribisha Afisa Elimu kuongea , Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kibiki ,Mwl Magreth Kileo ameshukuru ufadhiri huo na kusema kwamba kukamilika kwa madarasa hayo kutaondoa wanafunzi kupishana (session) na kufanya wanafunzi kuingia na kutoka kwa wakati mmoja.

Afisa elimu msingi wa halamashauri ya Chalinze, Bi. Miriam Kihiyo akizungumza na Wananchi katika viwanja vya shule ya msingi Kibiki. Katikati Ni mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi. Magreth Kileo na kushoto kabisa Ni kaimu Mwenyekiti wa kamati ya shule Bw. Hassan Mzee .
Diwani wa kata ya Bwilingu, Mh. Nassar Kalama akisisitiza jambo




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com