Mbunge wa Jimbo la Buyungu,Aloyce Kamamba akizungumza na wananchi
Daniel Limbe,Kakonko
MBUNGE wa Jimbo la Buyungu wilayani Kakonko mkoani Kigoma,Aloyce Kamamba,amewataka maofisa maendeleo ya jamii kwenda vijijini kuwaelimisha wananchi namna ya kuomba fedha za mikopo inayotolewa na halmashauri hiyo.
Uamuzi huo unatokana na malalamiko ya baadhi ya wananchi ambao wamemweleza Mbunge huyo kuwa wameshindwa kunufaika na fedha zinazotolewa na halmashauri hiyo baada ya maombi yao kukataliwa.
Alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Rumashi kata ya Nyabibuye wilayani humo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kuwashukuru kwa kumchagua kuwa mbunge wa jimbo hilo,pamoja na kukagua miradi ya maendeleo.
Awali akielezea kero waliyonayo wananchi hao,Gaston Mathayo,mkazi wa Kijiji hicho amedai hakuna wananchi walionufaika na mikopo ya aslimia 10 inayotolewa na halmashauri hiyo kutokana na vikundi vilivyoomba fedha kuambiwa maombi yao hayana sifa.
Akijibu malalaniko hayo, Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Steven Mabuga, amekana kuwepo kwa ubaguzi wa utoaji mikopo kwa walengwa badala yake amedai kuwa vikundi vingi wanawasilisha maombi pasipo kuzingatia maelekezo yanayotakiwa kisheria.
" Mheshimiwa Mbunge haya madai ya kuwa wananchi hawajanufaika na mikopo ya halmashauri siyo kweli...kuna vikundi viwili kwenye Kijiji hiki tayari wamepatiwa mikopo na wanaendelea kulejesha vizuri", amesema Mabuga.
Hata hivyo amekiri kuwa baadhi ya vikundi hawajui kuandika barua za maombi ya mikopo ya aslimia 10 kutoka halmashauri hiyo, huku baadhi ya vikundi vya wanawake wakiwa na wanachama wanaume jambo ambalo halikubaruki kisheria.
Kutokana na hali hiyo, Mbunge Kamamba,akalazimika kutoa maelekezo kwa idara ya maendeleo ya jamii kutoka maofsini kwenda kuwaelimisha wananchi namna bora ya kuandika barua za maombi ya mikopo badala ya kuzitupilia mbali pasipo kuwaelimisha.
"Bahati nzuri kaimu mkurugenzi upo hapa tena wewe ndiye mhusika wa ofisi ya maendeleo ya jamii...nakusihi muondoke ofsini mwende kuwafundisha hawa wananchi...haiwezekani maombi yao mnayakataa kwa sababu yamekosewa wakati bado hamjawaelimisha namna ya kuandika",amesema Kamamba.
Mikopo ya aslimia 10 hutolewa na halmashauri zote nchini huku aslimia 4 zikielekezwa kwa vikundi vya wanawake,aslimia 4 vijana na aslimia 2 walemavu.