Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO AAGIZA KUTAFUTWE MBINU MBADALA ZA KUWAFIKIA WAFUGAJI KATIKA UTOAJI WA CHANJO


 
****************** 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameagiza kutafutwe mbinu mbadala za kuwafikia wafugaji katika utoaji elimu ya chanjo kwa mifugo ili kuondokana na magonjwa hatari kwa wanyama. 

Mhe Dkt. Mpango ametoa maagizo hayo Agosti 1, 2022 wakati alipotembelea banda la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwenye ufunguzi wa Maonesho ya Wakulima na wafugaji Nanenane yaliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya kwenye viwanja vya John Mwakangale.

 "Tufike mahali haya magonjwa sijui kwato zimefanyaje, kimeta sijui na nini, tuwe na chanjo ambazo zimesambaa, hii itatusaidia sana wafugaji maana wanapoteza sana mifugo yao."

 “Vilevile tufike mahali lazima tuweke bima kwa wafugaji wetu ili baadae iweze kuwasaidia maana wanapata changamoto pindi mifugo inapokufa.”

 Amesema Dkt. Mpango Mhe Dkt. Mpango amewataka Wakala ya Maabara ya Veterinali Tanzania (TVLA) kuhakikisha usalama unakuwepo katika maabara zao ili kulinda afya za binadamu na hata wanyama. 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki alisema kuwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 Wakala imeongezewa fedha ili kufikia mwishoni mwa mwaka huu waongeze uzalishaji wa chanjo, asilimia zitakazobaki zitaagizwa nje ya nchi na kwa sasa Wakala ina aina saba za chanjo wanazozalisha na uwezo wake ni mzuri.

 “Mwaka huu tumepeta kibali cha kuajili maafisa mifugo wapatao 300, wote hao watakwenda kwenye Serikali za mitaa kwa ajili ya kuwafikia wafugagi, vilevile mwaka huu tumetenga bajeti ya pikipiki 1,300 ambazo zitakwenda kuwasaidia maafisa mifugo wetu kuwafikia wafugaji Tanzania nzima ili waweze kupata huduma za chanjo.” Alisema Mhe. Ndaki

 Akiogea kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Meneja wa Wakala kituo cha Iringa Dkt. Qwari Bura alisema kuwa Wakala ina lengo la kuzalisha aina 13 za chanjo za magonjwa, na hadi kufikia sasa Wakala imezalisha aina saba za chanjo. 

Chanjo hizo ni chanjo ya mdondo ya kuku, chanjo ya homa ya mapafu ya ngombe, chanjo ya homa ya mapafu ya Mbuzi, chanjo ya Kimeta, chanjo ya chambavu, chanjo ya homa ya kutupa mimba pamoja na chanjo ya mchanganyiko ya kimeta na chambavu, na kwa sasa uwezo wa kuzalisha chanjo umefikia asilimia 60 ya mahitaji ya nchi.

 Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania Inajihusisha na ufanyaji wa Uchunguzi wa Magonjwa ya Wanyama, Uzalishaji wa Chanjo za Wanyama, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, uhakiki wa ubora wa viuatilifu vya mifugo utafiti wa magonjwa ya mifugo pamoja na huduma za ushauri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com