Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema amewasihi wananchi wa kijiji cha Nyang’ombe kata ya Mwakitolyo kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajia kufanyika Agosti 23 ,2022 .
Mjema amesema hayo leo Agosti 10, 2022 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho uliokuwa na lengo la kuhamasisha umuhimu wa zoezi hilo pamoja na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kijiji hicho.
“Kuna umuhimu mkubwa wa kufanya sensa kwani itatoa takwimu muhimu ambazo Serikali itazitumia kufahamu mahitaji yenu wananchi na miundombinu inayotakiwa kuboreshwa ili muweze kupata huduma muhimu.
“Takwimu hizi tunaweza kuzitumia kwa maendeleo yetu wenyewe kuna masuala ya ujenzi wa vituo vya afya, madarasa, uwekezaji wa aina mabalimbali” alisema Rc Mjema.
Hata hivyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu kufanyika kwa sensa mwaka huu na maandalizi ya serikali ya kuwezesha bajeti ya masuala ya sensa .
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliojitokeza kwenye mkutano huo wamemshukuru Mkuu wa mkoa wa Shinyanga kwa kufika katika kijiji hicho kwani hawajawahi kupata kiongozi wa ngazi za juu kuja kusikiliza kero zao.
Pia wamemuahidi kuwa watashiriki vyema katika zoezi hilo kwani serikali imetoa elimu ya kutosha iliyowafanya kuelewa umuhimu wa zoezi hilo.