Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUENDELEA KUKUZA SEKTA YA UBUNIFU KUPITIA MAONI YA WADAU WA SAYANSI


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Caroline Nombo akizungumza wakati wa kupokea maoni ya wadau juu ya maboresho ya rasimu ya sera ya Sayansi, Teknolojia na ubunifu leo Jijini Dodoma


*****


Na Dotto Kwilasa,DODOMA

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imesema inaendelea  kupokea maoni ya wadau juu ya maboresho ya Rasimu ya Sera ya Sayansi ,Teknolojia na Ubunifu na Mfumo wa  Uratibu wa masuala ya ubunifu  ili kukuza sekta ya ubunifu.


Aidha kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi  imeendelea kuwekeza katika kujenga uwezo na mazingira rafiki nchini ili kuongeza kasi ya maendeleo na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kukuza uchumi, kuongeza pato la Taifa, na kuboresha maisha ya watanzania kwa ujumla.


Naibu Katibu Mkuu ,Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Caloline Nombo amesema hayo leo  jijini hapa wakati akifungua kikao kazi kinacholenga kuboresha sera hiyo huku akisisitiza kuwa ,wadau wanapaswa kutoa maoni yatakayoleta sera bora na mfumo utakaojibu matarajio ya ubunifu hapa nchini.


Amesema juhudi hizo, pamoja na mambo mengine, zinajumuisha kuandaa Sera, Kanuni, Miongozo na Mikakati madhubuti na inayoendana na kasi ya mabadiliko ulimwenguni kote na kukidhi mahitaji ya nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.


“Hii imekuwa ni dhamira yetu katika  kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu,aidha dhamira hii ni sehemu ya ajenda za nchi yetu toka miaka ya 1960, sambamba na kuanzishwa kwa Baraza la Taifa la Utafiti wa Sayansi (UTAFITI) mnamo mwaka 1968, na kutungwa kwa Sera ya kwanza ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (ST) ya mwaka 1985,"amesema Naibu Katibu Mkuu huyo.


Pia amesema, Sera hiyo ya mwaka 1985 ilifuatiwa na Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996 ambayo imetumika kwa kipindi chote hadi sasa na kwamba utekelezaji wa Sera hiyo na mikakati mingine ya kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu, vimesaidia kuimarisha maendeleo na matumizi ya Sanyansi na Teknolojia katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.


Prof. Nombo ametaja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa Taasisi za utafiti na maendeleo nchini kutoka 18 mwaka 1961 hadi kufikia jumla ya taasisi 94 mnamo mwaka 2021,kupandishwa hadhi kwa Chuo cha Ufundi cha Dar es Salaam na kuwa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (1997) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (2006) kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (2012).


Amefafanua kuwa ,kutokana na mafanikio hayo, vyuo hivi vimeongeza uwezo katika shughuli za kitaaluma na utafiti katika Sayansi na Teknolojia na kutolea mfano mwaka 2011 kwamba Serikali ilianzisha rasmi Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia kwa kuwa kitovu utafiti, ugunduzi na ubunifu wenye hadhi ya kimataifa.


"Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa Taasisi za Elimu ya Juu ambazo pia zinajihusisha na utafiti na ubunifu kutoka Chuo Kikuu kishiriki kimoja hadi kufikia Vyuo Vikuu 47 mwaka 2021,kuongezeka kwa Vituo vya bunifu na Atamizi hadi kufikia Vituo zaidi ya 45 kufikia mwaka 2022, na kuongezeka kwa idadi ya watafiti kutoka taasisi za elimu ya juu na taasisi za utafiti na maendeleo za umma kutoka 3,593 mwaka 2007/08 hadi 10,966 mwaka 2021,"amesema.


Pia kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia (MTUSATE) mwaka 1995 ambao hadi sasa mfuko huo umepokea zaidi ya shilingi bilioni 51.99,kuzalisha teknolojia mbalimbali zenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, uzalishaji wa mbegu mpya za mazao na wanyama, chanjo mpya za magonjwa ya mifugo, teknolojia rahisi za kusafisha maji ya kunywa na mtambo mdogo wa kuzalisha sukari .


Aidha amesema,mapitio ya sera ya mwaka 1996 yamebaini changamoto na mahitaji mbalimbali ambayo yamepelekea  kuhuisha Sera iliyopo ikiwa ni pamoja na kuandaa Kiunzi cha Uratibu wa Masuala ya Ubunifu nchini `National Innovation Framework' ambacho kinatumika kama nyenzo inayorahisisha utekelezaji wa Sera, pamoja na kuimarisha uratibu na usimamizi wa ubunifu katika ngazi mbalimbali na utengamano kati ya wadau mbalimbali wa sayansi.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolijia (COSTECH) Dkt. Amosi Nungu amesema kikao kazi hiyo ni cha muhimu hivyo
wadau wanapaswa kutoa maoni ambayo yatasaidia kuboressha Rasimu ya Sera ya Sayansi Teknolijia na Ubunifu wa mfumo wa Uratibu wa masuala ya Ubunifu hapa nchini.


Kufuatia hali hiyo Dkt. Nungu amesisitiza kila mshiriki wa kikao hicho kutoa maoni ili aweze kuisaidia serikali kuboresha Sera hiyo ambayo ni muhimu kwa taifa.


Naye Jerry Slaa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za jamii  ameipongeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kutokana na kutekeleza kikamilifu masuala ya Ubunifu,suala jambo ambalo litasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.


Sambamba na hayo amewataka kuendelea kuwaita wadau mbalimbali ili kuweza kubuni zaidi  vitu mbalimbali ambavyo vitasaidia kuwainua vijana kiuchumi.


Kwa upande wake Mwakilishi kutoka UNESCO Faith Shayo amesema wanafurahi kuwa katika warsha hiyo yenye lengo la kuleta wadau pamoja,kwa ajili ya kufanya mapitio ya rasimu ambayo yatazingatia pamoja na  masuala mengine kuhusu tafiti na watafiti wa kisanyasi.


Amesema Shirika la umoja wa mataifa (SIDA) wanashirikiana na Wizara ya  Elimu na Unesco kutekeleza mradi unaolenga kuimarisha maendeleo ili
kufikia malengo endelevu yanayotekelezwa nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com