SERIKALI YAWATAKA WENYE VIWANDA KUIJALI NA KUILINDA NGUVUKAZI


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, akikagua nyaraka mbali mbali katika moja ya viwanda alivyotembelea kwa lengo la kufuatilia utekeleza wa sheria za Kazi na Ajira. Alioambatana nao ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi-WCF (katikati) na Maafisa wengine wa OSHA, NSSF na Idara ya Kazi.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, akikagua vibali vya kazi vya wataalam wa kigeni katika moja ya viwanda alivyotembelea kwa lengo la kufuatilia utekeleza wa sheria za Kazi na Ajira.


Kaimu Meneja wa Kanda ya Pwani wa OSHA, Mhandisi George Chali, akiainisha mambo waliyoyabaini wakaguzi wa OSHA wakati wa ziara mbele ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi pamoja na wafanyakazi wa viwanda vilivyotembelewa. Baadhi ya changamoto za usalama na afya alizozieleza ni pamoja na ukosefu wa vifaa kinga miongoni mwa wafanyakazi, uwepo wa nafasi finyu za kufanyia kazi na mifumo ya umeme isiyozingatia usalama.


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, akiwa ameambatana na Mkurugenzi WCF, Dkt. John Mduma (katikati) na Maafisa wengine wa OSHA, NSSF na Idara ya Kazi wakati ziara yake katika viwanda iliyolenga kufuatilia utekeleza wa sheria za Kazi na Ajira.


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi, akiongoza kikao cha maandalizi ya ziara yake katika viwanda kilichofanyika katika Ofisi za OSHA jijini Dar es Salaam.

**************************

Na Mwandishi Wetu

Serikali imewataka wamiliki wa viwanda nchini kuijali na kuilinda nguvukazi inayotumika katika uzalishaji ili kuwa na uzalishaji endelevu na wenye tija kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Tamko hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, alipofanya ziara katika viwanda mbali mbali jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na Maafisa wa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwemo Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).

Akizungumza katika ziara hiyo, Katambi amesema malengo ya serikali ya awamu ya sita ni kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia uzalishaji viwandani ambapo serikali inawajibika kujenga mazingira bora ya biashara na uwekezaji.

“Sisi kama serikali tunajitahidi kuhakikisha kwamba kunakuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kuhakikisha kwamba shughuli zote za uwekezaji zinazingatia sheria za nchi ikiwemo sheria za Ajira na Mahusiano Kazini, Usalama na Afya Mahali pa Kazi na hifadhi kwa jamii,” amesema Naibu Waziri na kuongeza:

“Katika ziara hii ya leo tumefanya ukaguzi wa kushtukiza katika viwanda vitano vinavyozalisha bidhaa mbali mbali zikiwemo bidhaa za plastiki ambapo tumebaini mapungufu mengi katika viwanda husika ikiwemo mazingira ya kazi yasiyo rafiki kwa wafanyakazi na uwepo vitendo vya unyanyasi kwa wafanyakazi. Hivyo, nitoe rai kwa waajiri wote nchini kuhakikisha kwamba wanatoa ajiri zenye staha ili kuendana na sheria za nchi pamoja na miktaba ya kimataifa ambayo nchi yetu imeiridhia.”

Aidha, Katambi amewakaribisha wawekezaji wenye changamoto mbali mbali katika shughuli zao kuziwalisisha changamoto hizo serikalini ili ziweze kupatiwa ufumbuzi na hivyo kuondokana na vikwazo katika uzalishaji.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kanda ya Pwani wa OSHA, Bw. George Chali, ameainisha changamoto za usalama na afya zilizobainika katika ziara hiyo zikiwemo ukosefu wa vifaa kinga miongoni mwa wafanyakazi, uwepo wa nafasi finyu za kufanyia kazi, wafanyakazi kutekeleza majukumu yao katika mtindo usiofaa kiusalama na afya (ergonomic issues).

Masuala mengine ni mifumo ya umeme isiyozingatia usalama, zana na mitambo ya kazi isiyozingatia kanuni za usalama, viwango duni vya mwanga katika maeneo ya kufanyia kazi, viwango vya juu vya kelele za mashine pamoja na ukosefu au uwepo wa huduma duni za kijamii mathalani vyoo, vyumba vya kubalishia mavazi, sehemu za kulia chakula pamoja na ukosefu wa maji safi na salama ya kunywa katika sehemu za kazi.

Kutokana na mapungufu yaliyobainika, Naibu Waziri ameziagiza Taasisi zinazohusika na changamoto hizo zikiwemo OSHA, NSSF, WCF na Idara ya Kazi kuviandikia viwanda vilivyotembelewa maboresha yanayohitajika na kufuatilia kwa karibu kuhakikisha kwamba yanafanyika kwa haraka.

Ziara hizo ambazo ni endelevu zinafanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu katika maeneo mbali mbali ya kazi nchini lengo likiwa ni kufuatilia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini pamoja na Sheria za Hifadhi kwa Jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post