Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YAPOKEA EURO MILIONI 10 KUTOKA SERIKALI YA UJERUMANI KWA AJILI YA MIRADI YA MAENDELEO


******************

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea fedha kiasi cha Euro Milioni 10 kutoka kwa Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na mradi wa kupunguza migogoro baina ya binadamu na Wanyamapori ambao una thamani ya Euro milioni 6.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Juma S. Mkomi wakati wa hafla fupi ya Kusaini Makubaliano Baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya Utekelezaji wa Miradi hiyo katika ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu leo jijini Dar es Salaam.

“Fedha hizi tulizopokea kiasi cha Euro Milioni 6 zinalenga kutekeleza Mradi wa Kupunguza Migogoro baina ya Binadamu na Wanyamapori katika wilaya mbalimbalii lakini hasa katika wilaya 88 ambazo zipo karibu na maeneo yaliyohifadhiwa” Bw. Mkomi amesisitiza.

Amefafanua kuwa katika wilaya za Serengeti, Bunda Vijijini, Tunduru, Mwanga, Mvomero, Namtumbo na Itilima kumekuwa na matukio mengi ya wanyamapori kusababisha madhara kwa wananchi na mazao ukilinganishwa na wilaya nyingine.

Amesema hali hiyo imesababisha hasara kubwa kwa wananchi, akitolea kwa mfano katika kipindi cha miaka mitano (2017 - 2021), wastani wa wananchi 28,137 wamepata madhara kutokana na wanyamapori ikijumuisha uharibifu wa mazao (ekari 56,972) yenye thamani ya wastani wa shilingi bilioni 28, jumla ya wananchi 508 kujeruhiwa na 634 kuuawa na wanyamapori.

Ameweka bayana kuwa mradi huo utakuwa na mchango mkubwa katika kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori nchini na kuihakikishia Serikali ya Ujerumani kwamba fedha hizo zitatumika kwa lengo lililokusudiwa na si vinginevyo.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani kwa misaada inayoendelea kuitoa hususan katika maeneo yanayohusiana na uhifadhi wa maliasili.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Balozi wa Jamhuri ya Shiikisho la Ujerumani, Mhe. Bi. Regine Hess, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango,Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria; Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii,Viongozi wa GIZ pamoja na Maafisa wa Serikali za Tanzania na Ujerumani.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com