NAIBU Mrajis wa Vyama vya Ushirika kutoka tume ya maendeleo ya ushirika Bw. Collins Nyakunga ,akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la tume hiyo kwenye maonyesho ya 88 yanayofanyika Nzuguni Jijini Dodoma kuelezea mipango mbalimbali inayofanyika na tume hiyo.
NAIBU Mrajis wa Vyama vya Ushirika kutoka tume ya maendeleo ya ushirika Bw. Collins Nyakunga akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari kwenye banda la tume hiyo kwenye maonyesho ya 88 Jijini Dodoma kuelezea mipango mbalimbali inayofanyika na tume hiyo.
Baadhi ya wananchi waliofika katika banda la tume ya maendeleo ya ushirika jijini Dodoma wakipata elimu ya ushirika katika maonyesho ya 88 kanda ya kati Jijini Dodoma.
..................................
Na Alex Sonna-DODOMA
TUME ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) inatarajia kuanza kutumia Mfumo wa kielekroniki katika kusajili wanachama katika vyama vya ushirika ili kudhibiti na kuongeza uwazi katika usimamizi wa vyama vya ushirika na kuondoa changamoto ya Usimamizi katika Vyama vya Ushirika Nchini.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma leo Agosti 03, 2022 kwenye Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati na Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Collins Nyakunga ambapo amesema lengo la kusajili Vyama na wanachama kwa njia ya kielektroniki ni kuongeza Usimamizi kwenye vyama hivyo.
“Ushirika ni sehemu inayowanufaisha wananchi katika shughuli zao za kilimo, uvuvi na mifugo kwa kutambulika na kulinda maslahi ya wananchi kwa kuwasajili kidigitali ili mchango wao katika maendeleo ya nchi uweze kufahamika,” amesema Nyakunga.
“Kulikuwa na changamoto katika kuwafikia wanachama kwenye Vyama vya Ushirika na hivyo kufanya ukaguzi kuwa mgumu maana Maafisa Ushirika waliopo sio wengi lakini sasa tutavifikia kupitia Mfumo wa kielekroniki na kuvikagua kirahisi,” amesema.
Kupitia usajili kwa njia ya TEHAMA vyama vyote vitatambulika na itakuwa rahisi kufahamu mchango wa Ushirika katika Pato la Taifa na hakutakuwa na ugumu kupata takwimu na taarifa za Ushirika.
Amesema kwenye Ushirika kuna manufaa makubwa tofauti na kusimama Mvuvi, Mfugaji au Mkulima akiwa peke yake kwa kuwa hataweza kupata nguvu ya Soko la bidhaa zake.
Amebainisha kuwa awali zao la Kakao kilo moja ilikuwa inanunuliwa Shilingi 1,800 lakini mara baada ya kuanza kuuzwa kupitia Mfumo wa Ushirika, bei imepanda hadi kufika zaidi ya Shilingi 5,000.
“Miaka ya nyuma, kwenye zao la Korosho kulikuwa na udanganyifu wa vipimo na bei ilikuwa ndogo sana, lakini baada ya Mfumo wa Ushirika kuanza kutumika sasa bei ni zaidi ya Shilingi 1,600, 2,000 hadi 3,000 kwa kilo moja, haya ndio manufaa ya Ushirika shirika” amesema Naibu Mrajis wa Vyama vya Ushirika.
Social Plugin