Na Daniel Limbe,Kakonko
KATIKA kile kinachoonekana ni kukabiliana na uharifu wa mazingira nchini, Mbunge wa jimbo la Buyungu mkoani Kigoma,Aloyce Kamamba, amewataka wakazi wa kijiji cha Kinyinya kata ya Nyamtukuza,kuacha kukata ovyo miti ya asili kwa lengo la kuweka makazi,kukata mkaa,kupasua mbao, kuchimba madini na kilimo cha kuhama hama.
Ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kinyinya wakati akihamasisha maendeleo kwenye jimbo lake huku akiwasisitiza kutunza chakula badala ya kuuza ili kukidhi mahitaji mengine.
"Niwatake muache kukata miti ovyo...kama ni ujenzi wa shule muondoe miti kwenye eneo linalohitajika pekee...lengo letu ni kuhifadhi uoto wa asili,kuvutia mvua na kulinda uhai wa viumbe wengine". amesema Kamamba.
Mbali na hilo,amewataka kuhifadhi mazao ya chakula na kuongeza kilimo cha kibiashara, sambamba na kuwataka kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa kwenye sensa ya watu na makazi ili kusaidia jitihada za serikali kusogeza maendeleo kwa uwiano wa watu waliopo eneo husika.
"Ndugu zangu sensa ni muhimu sana kwa maendeleo yetu...niwasihi mjitokeza kwa wingi hata kama kuna mtu ambaye siyo raia wa Tanzania lakini yupo kwako hakikisha anahesabiwa"
Kadhalika amesisitiza kutowaficha ndani watoto wenye ulemavu badala yake wapewe kipaumbele kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.
Mbali na kumpongeza Mbunge huyo kwa kusaidia miradi ya maendeleo kwa jamii, Erasto Kweyunga, ameitaka serikali kuwasogezea huduma za nishati ya umeme na gesi ili waepukane na uharibifu wa mazingira hasa ukataji mkaa kwaajili kupikia.
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kakonko, Steven Mabuga, amewataka wananchi hao kutunza mazingira ili kunusuru uhai wao na viumbe hai wengine.