Nyanya
Na Mwandishi wetu - Mwanza
Wataalamu wa kilimo cha asili (Kilimo Hai) wameshauri kuzalisha mbegu za asili na kuzalisha mbegu zake za asili wakieleza kuwa ardhi ni kila kitu na ikichezewa inakufa.
Akitoa maelezo ya jinsi ya kutengeneza mbolea ya asili na viuadudu kwa kutumia miti na bidhaa zingine ambazo ni za asili, kwenye maonesho ya Nane Nane katika viwanja vya Nyamhongolo kwa wananchi waliotembelea banda la GBM Tanzania Organic Farming For Better Health, Mtaalamu wa Hai, James Kalokola kutoka taasisi hiyo isiyokuwa ya kiserikali ya GBM amesema amezitaja faida za kilimo hicho kuwa ni pamoja na kilimo hicho ni bora kwa afya ya mmea na wanadamu, wanyama, mazingira na afya udongo.
Amesema Maeneo mengi ya ardhi yamekufa yanahitaji kufufuliwa, ardhi imekufa kwa sababu microbio ambao wanachakata udongo na kutengeneza chakula kwa ajili ya mimea vimepungua sana ama hazipo na ndiyo maana ya kusema ardhi au udongo hauna rutuba.
Akielezea jinsi ya kutengeneza mbolea na viuatilifu hai hivyo, Mtaalamu wa Kilimo Hai Peter Mlay amesema Kilimo Hai mazao yake yanazalishwa kwa mfumo wa bei nafuu na soko lake lipo hususani kwa nchi za Ulaya na Marekani.
“Soko liko wazi sana bado hatutajajisumbua kulitafuta, tunachokihitaji ni kuboresha vifungashio na uhifadhi wa mazao yasiharibike kabla ya kufika sokoni.
“Faida nyingine amesema gharama za uzalishaji kwa njia hii zipo chini. Kilimo hiki hakihitaji mbolea ya viwandani na wala viuatilifu vya viwandani wala mbegu za Hybrid kwani kinachohitajika ni mbegu za asili na mbegu hizo za asili kwa kutumia mbolea hiyo ya asili vinatoa mazao ya kutosha”, alisema
“Kule Kilimanjaro kuna wakulima wametumia mbolea hizi na viuadudu pamoja na mbegu za asili, wamepata wastani wa magunia kati ya 18 na 22 kwa heka. Wakulima hawa wapo Sanya Juu na kule karibu na Hospitali ya KCMC. Na wakulima wa mpunga huko Moshi walitumia mbolea hizi hata ladha ya mchele wao ilibadilika na kufananishwa na mchele kutoka Mbeya”,alisema
“Kilimanjaro tuliitwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo marehemu Anna Mghwira na kwa sasa tupo na Kanisa la KKKT Ushirika wa Neema Moshi ikiwa ni eneo la Pilot na Training.
Ombi letu kwa serikali, tunaomba serikali yaani Waziri wa Kilimo atupe nafasi ya kuonana naye ili tueleze package nzuri tulizonazo ambazo tunaamini zitachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza tija katika kilimo. Tunahitaji mkakati wa kukusanya na kuhifadhi mbegu pia”,aliongeza.
Amesema Mbegu za asili zinaweza zikapotea lakini kama zikihifadhiwa mbegu hizi hazitapotea.
“Tukisema kila wilaya ihifadhi na kuzalisha mbegu zake za asili itawezekana na hii inawezekana. Tufanye hivyo kwani nchi zingine zinafanya baada ya kuona mbegu zake za asili zinapotea, tukifanya hivyo tutakwenda kuokoa dunia kwani tuna kila kigezo cha kufanikisha hili, tufunguke macho ”,alisisitiza mtafiti huyo
Naye ndugu Michael C Park ambaye ni Mtafiti wa masuala ya Kilimo kutoka Korea Kusini amesema :
“Mungu ana mpango mwema na nchi hii, na hili litasaidia nchi za Afrika na dunia kwa ujumla. Tunahitaji kuzalisha bidhaa hizi ili wananchi wazipate kwa gharama ndogo ‘kwa gharama ya uzalishaji –production costs. Pili nchi ipate Benki ya mbegu za asili ambazo zinapotea sasa jambo ambalo siyo salama kwa uasili wa mwanadamu.
Tatu Mwezi Oktoba tutakuwa na mafunzo maalumu mkoani Kilimanjaro tunawakaribisha wataalamu wa kilimo waje wajifunze teknolojia hii ambayo kwa nchi hii ni mpya. Leo tupo hapa kwenye maonesho ya Nane Nane tumealikwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuja kutoa elimu na kuwaeleza wananchi kuwa tunatarajia kuzalisha mbolea ya kimiminika na kwa kutumia mabaki ya samaki ambayo yanabaki kwenye viwanda vya samaki hapa mkoani Mwanza”,alisema Mtafiti huyo ambaye amefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita na umri wa zaidi ya miaka 80.
Social Plugin