Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UJENZI BWAWA LA NYERERE WAFIKIA 67%, KAZI USIKU NA MCHANA


Waziri wa Nishati, January Makamba akiwa na Bodi na Menejimenti ya TANESCO pamoja na Wahariri wa Vyombo mbalimbali wakikagua hatua za ujenzi zilizofikiwa katika mradi wa umeme wa Julius Nyerere.

***************************

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2,115 umefikia asilimia 67.

Makamba alieleza hayo 8/8/2022, mbele ya wajumbe wa bodi ya TANESCO, Wahariri na wanahabari wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea mradi huo kujionea hatua iliyofikiwa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa Waziri Makamba, moja ya sababu za mafanikio haya ni ujenzi kufanyika usiku na mchana, jambo ambalo limeongeza kasi kwa kiwango kikubwa.

“Kasi kubwa ya ujenzi inaendelea katika mradi huu. Sasa hivi kazi inafanyika saa 24 usiku na mchana. Mtakuwa mashahidi leo ikiwa ni sikukuu ya Nanenane lakini watu wapo kazini na wanabadilisha zamu tu,” alisema Makamba.

Sababu nyingine aliyoelezea Waziri Makamba ni maboresho na mabadiliko yaliyofanyika katika Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na bodi yake ambazo zimekuwa zikifuatilia ujenzi wa bwawa hilo na kuwasimamia makandarasi kwa ukaribu.

Akifafanua hatua hii iliyofikiwa, waziri Makamba alisema “ukitazama maendeleo ya mradi, miaka miwili na nusu ya mwanzo toka Disemba 2018 mpaka Juni 2021, tulifikia asilimia 37. Leo tuko asilimia 67 (ongezeko la takriban mara mbili chini ya mwaka mmoja). Ni kasi kubwa katika kipindi kifupi”.

Katika ziara hiyo, wahariri na wanahabari walipata fursa ya kujionea maeneo nane muhimu katika mradi huo ikiwemo ujenzi wa tuta kuu (main dam) ambalo Juni 2021 ulikuwa asilimia 26 lakini hadi hivi sasa asimilia 78. Daraja la kudumu (permanent bridge) ambalo ni muhimu kupitisha vifaa vya ujenzi vyenye uzito mkubwa, ujenzi wake Juni 2021 ulikuwa asilimia 37.8, hivi sasa asilimia 95.

Pia, walijionea njia za maji kuendesha mitambo (power water ways) ambazo ujenzi wake kuanzia Juni 2021 ulikuwa asilimia 43 sasa hivi upo 85. Jengo la mitambo (power house) Juni 2021 lilikuwa asilimia 29, sasa asilimia 51. Kituo cha kusafirishia umeme (switchyard) hadi Juni 2021 kilikua asilimia 38, sasa hivi asilimia 89.7.

Kabla ya kuanza kwa ziara hiyo ya kutembelea maeneo mbalimbali ya mradi, wahariri na wanahabari walipata fursa ya kuonyeshwa picha na video fupi za maendeleo ya mradi huo – hatua ambayo iliwafungua macho wengi kujionea kasi na ukubwa wa kazi iliyofanyika ndani ya mwaka mmoja.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema , "tulikuwa tunasikia tu mradi unaendelea lakini hatukuwa na taarifa sahihi lakini leo (juzi), tumeona. Tunashukuru na kupongeza hatua iliyofikiwa kwenye mradi huu," alisema.

Katika ziara hiyo, waziri Makamba pia alikutana na kuongea na mafundi ujenzi wanaotekeleza mradi huo. Pamoja na kumueleza waziri changamoto zao na mambo ambayo wangependa ayafanyie kazi, pia mafundi hao walieleza wanavyojivunia kushiriki ujenzi wa mradi huo wa kitaifa.

 “Tunajivunia kama vijana wa kitanzania kuwa sehemu ya mradi huu wa kihistoria nchini kwetu. Sasa unakwenda kwa kasi kubwa, vifaa vinafika kwa wakati na usimamizi umekuwa bora zaidi,” walisikika wakimueleza waziri Makamba.

Bwawa la Nyerere linajengwa katika maporomoka ya mto Rufiji mkoa wa Pwani. linatarajiwa kuzalisha megawati 2115, zitakazoingizwa kwenye gridi ya Taifa ili kuongeza, kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com