Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKULIMA DODOMA WASHAURIWA KUTUMIA HUDUMA ZA MAWASILIANO KUPATA FURSA ZA KILIMO NA MASOKO

Na Mwandishi Wetu

Wakulima mkoani Dodoma hasa wanaojihusisha na kilimo cha zao la Zabibu wamesisitizwa kutumia fursa zinazopatikana kwenye mtandao kupata taarifa sahihi zitakazowezesha kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji wa kilimo, sambamba na kupata fursa na taarifa za masoko.

Akizungumza katika banda la maonesho la Mamlaka hiyo kwenye maonesho ya kilimo mkoa wa Dodoma Meneja TCRA Kanda ya Kati Boniface Shoo alisisitiza kuwa elimu ya kutosha inayowezesha ukuzaji tija katika shughuli za kilimo katika zama za sasa inapatikana kwenye mtandao.

“Katika anga la mtandao tunazo fursa nyingi sana zinazowezesha wakulima hasa wakulima wa mkoa wetu wa Dodoma wanaojishughulisha na kilimo cha Zabibu kupata elimu ya kila namna kuhusu kilimo bora; TCRA tunawasisitiza wakulima kutembelea majukwaa ya kimtandao kupata elimu hii muhimu. Pia kubwa zaidi ni kupata mwanga wa mwenendo wa masoko ya bidhaa za mazao yao hasa Zabibu,” alibainisha Shoo.Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kati Bw. Boniface Shoo akiwa na Afisa Mawasiliano Bw. Robin Ulikaye katika mahojiano kwenye kituo cha utangazaji kufikisha elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi na salama ya Mawasiliano. Picha na: TCRA

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni miongoni mwa taasisi mbalimbali zilizoshiriki maonesho ya wakulima Kanda ya Kati ikinuia kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma za Mawasiliano hasa katika kuripoti matukio ya utapeli mtandaoni, kuhakiki usajili wa namba za Mawasiliano ya simu na matumizi sahihi na salama ya huduma za mtandao.



Afisa Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Robin Ulikaye akizungumzia kampeni hiyo alibainisha kuwa, wanalenga kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa kuepuka matukio ya utapeli kwenye mtandao, na wakati wote wanapotumia Mawasiliano.



“Mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu mara anapopokea ujumbe wa kitapeli au kupigiwa simu ya kitapeli kwenye mtandao wake wa mawasiliano, tunamshauri atoe taarifa juu ya utapeli huo kwa kutuma neno ‘utapeli’ kwenda namba 15040 kisha atapokea ujumbe unaomtaka kuwasilisha namba iliyomtumia ujumbe wa kitapeli; awasilishe namba hiyo na kikosi-kazi maalum kitapokea taarifa hiyo na kuifanyia kazi,” alibainisha Ulikaye.



Afisa huyo alisisitiza kuwa kutoa taarifa za utapeli hasa kwa jumbe za “ile pesa tuma kwenye namba hii…” kunasaidia kupunguza matukio ya utapeli mtandaoni.



“Pia tunawaomba wananchi wanaotumia huduma za Mawasiliano ya simu wahakikishe wanahakiki namba zao za simu zilizosajiliwa kwa namba za Kitambulisho cha Taifa ili wasalie kuwa salama wakati wote wanapotumia Mawasiliano; uhakiki wa laini za simu zilizosajiliwa kwa kitambulisho chako ni muhimu kwani unaepusha utambulishi wako kutumiwa na mtu mwingine, hasa isivyo halali” alibainisha na kuongeza.



TCRA ilibainisha kuwa zoezi la uhakiki wa Mawasiliano linakamilika kwa kubofya alama ya nyota Mia Moja na Sita kisha alama ya reli ambapo mtumiaji atafuata maelekezo na ikiwa kuna namba asizozitambua au kuzihitaji anaweza kuzifuta kwa usaidizi wa mtoa huduma wake wa Mawasiliano.



Kuhusu udhalilishaji mtandaoni Mamlaka hiyo ilisisitiza kuwa mtu yeyote anapotendewa udhalilishaji kwenye mtandao anapaswa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ambayo ni Jeshi la Polisi ili hatua stahiki za Kisheria ziweze kuchukuliwa.



Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni taasisi ya Serikali yenye jukumu la kusimamia sekta za Mawasiliano na Utangazaji Tanzania. Ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya mwaka 2003 kusimamia huduma za kielektroniki na posta na masafa ya mawasiliano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mamlaka ilianza kazi tarehe 1 Novemba 2003 na inafanya shughuli za zilizokuwa Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC) na Tume ya Utangazaji Tanzania (TBC).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com