Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAKULIMA WAFUNDWA JUU YA SUMUKUVU MAONESHO YA NANENANE MBEYA

Maafisa wa TBS wakitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la TBS katika maonesho ya wakulima nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale . TBS imeshiriki maonesho hayo na kutoa elimu kwa wananchi,wajasiriamali, wafanyabiashara,wakulima na wadau wa kilimo juu ya masuala ya udhibiti ubora kwa ujumla.

***************************

Wakulima na wasindikaji hususani wa mazao ya mahindi na karanga wameshauriwa kufuata kanuni bora za kilimo na usindikaji ili kuzuia mashambulizi ya kuvu na uchafuzi wa sumukuvu katika Mazao hayo na bidhaa zake kwa kuwa sumukuvu ina madhara makubwa kwa afya ya binadamu.

Wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti kuanzia tarehe 1 mwezi Agosti mpaka leo na maofisa wa TBS, kwa wakulima na wasindikaji waliotembelea banda la TBS katika maonesho ya wakulima nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale.

Afisa Usalama wa Chakula, Bw. Peter Namaumbo alisema TBS imeshiriki maonesho hayo ili kutoa elimu kwa wakulima,wafanyabiashara wa Mazao, wasindikaji wa bidhaa mbali mbali za chakula na wananchi kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uthibitishaji ubora wa bidhaa kwa wadau wanaosindika au kuongeza thamani kwenye bidhaa zao.

 Namaumbo alisema wakulima Wafanyabiashara na wasindikaji wa mazao ya nafaka hususani mahindi na Karanga wakidhibiti kuvu na sumukuvu itawawezesha kukuza uchumi,kupanua wigo wa Soko na kulinda Afya za mifugo na binadamu bila kusahau kuongeza utoshelevu wa chakula salama nchini .

Alitaja faida nyingine kuwa kuhimili ushindani katika masoko ya ndani, kikanda na nje ya nchi.

Akizungumza katika maonesho ya wakulima nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale Namaumbo, alisema sumukuvu huathiri zaidi mazao ya mahindi na karanga ambayo ni sehemu muhimu ya chakula cha Watanzania hapa nchini. "Kwa sababu hiyo sisi sote tunatakiwa kuzingatia mikakati ya kukabiliana na sumukuvu ili vyakula vyetu viendelee kuwa salama kwa muda wote," alisisitiza Namaumbo.

Alifafanua kwamba anatambua nafasi ya wakulima na mchango wao walionao, hivyo TBS imeshiriki maonesho hayo mahususi kwa ajili ya kutoa elimu ya udhibiti sumukuvu kabla ya kuvuna na baada ya kuvuna mazao.

Alisema umuhimu huu unasabisha suala la usalama wa chakula kupewa kipaumbele katika kulinda afya ya jamii, kukuza uchumi wa nchi na biashara kitaifa na kimataifa.

Alihimiza wakulima hao kuzingatia ushauri wa wataalam wa Kilimo na chakula ili kudhibiti sumukuvu kuanzia shambani, wakati wa kuhifadhi na kusindika kama inavyoshauriwa na wataalam katika chakula, ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni bora za kilimo kama inavyoshauriwa na wataalam.

Baadhi ya kanuni bora za Kilimo ni kuvuna Kwa wakati, kuepuka kurundika mazao chini, kwenye sakafu, kuhakikisha wanahifadhi vizuri mazao na kuepuka wadudu waharibifu, wanyama, joto kali na unyevunyevu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com