Meneja miradi kutoka shirika la ATFGM Masanga Valerian Mgani
Na Frankius Cleophace Tarime.
Watoto 1,036 wenye ulemavu katika wilaya ya Tarine wameibuliwa kwenye jamii na kuendelea kupewa elimu ili waweze kutambua haki zao.
Akizungumzia suala hilo Meneja miradi kutoka shirika la ATFGM Masanga Valerian Mgani alisema kuwa lengo la shirika ni kuibua watoto wenye ulemavu pamoja na wazazi na walezi na kupewa elimu juu ya haki za watoto.
"Kwenye jamii bado watoto wenye ulemavu wanatengwa hivyo hawapelekwi shule wanafichwa, sasa kupitia mradi wetu tumeanza kuibua watoto hai na kuwakutanisha pamoja ili kuweza kuwasaidia katika wilaya ya Tarime na Butiama", alisema Valerian.
Ikumbukwe kuwa kila mtoto anapozaliwa anapaswa kuishi, kupata elimu, kupewa mavazi na mahitaji yote hivyo jamii iondokane na suala la kutenga watoto wenye Ulemavu.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji kata ya Sirari Halmashauri ya wilaya ya Tarime, Atanaz Mwita alisema kuwa kuwa serikali sasa ione haja kubwa ya kuwekeza katika shule za watoto maalumu ili waweze kupata haki zao za elimu .
Atanaz aliongeza kuwa katika kata ya Sirari hakuna shule hata moja inayohudumia watoto wenye Ulemavu hivyo watoto hao wanalazimika kuchanganywa na wanafunzi wa kawaida jambo ambalo linatajwa kuwa changamoto kubwa.
"Mfano watoto wenye uoni hafifu, watoto wasiosikia wanapaswa kuwa na walimu wao lakini kata yangu ya Sirari hakuna shule hata moja wazazi wanalazimika kuchanganywa wototo anafika darasa la saba hajui chochote sasa serikali iweze kulitazama hilo", alisema Atanaz.
Aidha Msimamizi wa Miradi ya Terredes homes Netherland Lydia Kaugi alisisitiza watoto wenye ulemavu nao kuhesabiwa ifikapo Agosti 23 Mwaka huu wakati wa Sensa ya watu na Makazi.
Nao wazazi na walezi wameeleza kuwa bado kuna changamoto kubwa kwenye jamii ya kuficha watoto wenye Ulemavu hivyo serikali iendelee kutoa elimu ili watoto wawezekupewa haki zao za msingi.