Na Englibert Kayombo WAF, Dar Es Salaam.
WAZIRI wa Afya nchini Ummy Mwalimu leo amekutana na kufanya mazungumzo na Wawekezaji kutoka India pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu kujadili na kuwakaribisha kuona fursa za uwekezaji katika Sekta ya Afya nchini.
Waziri Ummy amepongeza nchi hizo kwa kuonyesha nia ya kutaka kuwekeza kwenye Sekta ya Afya na kuongeza ushirikiano katika kusaidia maendeleo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha ubora wa huduma za afya.
“Tumekuwa tukishirikiana na India kwenye mambo mengi kuhusu Sekta ya Afya, tuna madaktari wetu watanzania wanasoma masuala ya udaktari huko India, tuna wawekezaji kutoka India hapa nchini, ushirikiano huu ni mzuri na una tija kwa Serikali na Watanzania”,amesema
Waziri Ummy amesema kuwa kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Sekta ya Afya ni ubora wa huduma, hivyo kuwakaribisha wawekezaji hao kuwekeza hapa nchini ili Watanzania na raia kutoka nchi jirani waweze kupata huduma za kibingwa za matibabu.
Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa wawekezaji hao kuweka mkazo zaidi katika fursa za uwekezaji kwenye upande wa kuboresha mifumo ya TEHAMA kwenye Sekta ya Afya nchini huku akisema kuwa bado kuna changamoto nyingi kwenye mifumo ya TEHAMA ndani ya Sekta ya Afya.
Kwa upande wa Kiongozi wa wawekezaji kutoka India Lav Aggarwal amesema kuwa lengo la kufika nchini ni kuboresha zaidi ushirikiano baina ya nchi husika na wanatarajia kuendela kushirikiana na Tanzania katika kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma bora za matibabu hapa nchini.
Naye Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu hapa nchini Khalifa Al Marzooqi amesema ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika Umoja wa Falme za Kiarabu imefungua zaidi milango ya uwekezaji kutoka Falme za Kiarabu na kufika hapa kuja kuona nini cha kuwekeza kwenye Sekta ya Afya.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya prof. Abel Makubi amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya inafanya ushirikiano na taasisi mbalimbali za afya kutoka India na UAE kwenye Sekta ya Afya.
Prof. Makubi amewakaribisha pia wawekezaji hao kwenye upande wa uzalishaji wa dawa huku akisema kuwa Tanzania ina malengo ya kuzalisha dawa hapa nchini hvyo.
Mbali na hayo amepongeza ushirikiano ulipo kwenye masuala ya kuendeleza taaluma na kusema kuwa wapo watanzania wengi wanaojiendelea kitaaluma katika nchi hizo mbili kwenye masuala mbali mbali ya Sekta ya Afya.
Social Plugin