Afisa Mkuu wa Uwendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile (wapili kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mashine mpya na ya kisasa ya kuweka pesa ( Deposit ATM) katika hafla fupi iliyofanyika kwenye tawi ya Benki ya CRDB, Mlimani city jijini Dar es salaam. Wengine pichani ni Mkuu wa Kitengo cha Uwakala wa Kibenki wa Benki ya CRDB, Erick Willy (wapili kushoto), Kaimu Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Mashariki, George Yateta (kulia) pamoja na Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Mlimani City, Zaituni Manoro.
---
Wateja wa Benki ya CRDB sasa kupata huduma ya kuweka fedha masaa 24 kupitia ATM za kisasa za kuweka pesa. Hayo yameelezwa leo na Afisa Mkuu Uendeshaji wa Benki hiyo, Bruce Mwile wakati akizindua huduma hiyo katika tawi la Benki ya CRDB Mlimani City.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mwile alisema mashine hiyo inatumia teknolojia ya kisasa ambayo inawawezesha wateja kuweka pesa wenyewe bila usaidizi kwa urahisi, usalama, na unafuu. Mwile alisema mashine hizo zinauwezo wa kupokea hadi shilingi milioni 100 kwa mara moja.
“Tunatambua zipo biashara ambazo zinaendeshwa nje ya muda wa kazi wa kawaida ambapo matawi ya Benki na hata CRDB Wakala wanakuwa wamefunga, mashine hii inakwenda kutatua changamoto hii kwani huduma ya kuweka pesa sasa itapatikana masaa 24 kwa urahisi na usalama zaidi,” alisisitiza.
Pamoja na msisitizo wa mifumo ya kidijitali, ukweli ni kuwa matumizi ya fedha taslimu ‘noti na sarafu’ bado ni makubwa. Hii inaifanya huduma ya kuweka pesa “deposit” kuwa moja ya huduma muhimu za kibenki. Mashine hii ya kisasa ya kuweka pesa iliyozinduliwa na Benki ya CRDB inatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kihuduma.
Akieleza namna ya kutumia mashine hiyo Mwile alisema: “Mteja atatakiwa kuchagua lugha anayopenda kati ya kiswahili na kingereza, kisha ataweka TemboCard yake na kuingiza namba ya siri. Mteja ataweka pesa hadi noti 200 na kisha kubonyeza kitufe cha ‘Weka Pesa’, kisha utapokea taarifa kupitia ujumbe mfupi.”
Mwile aliongezea kuwa pamoja na kuzindua mashine hiyo katika tawi la Mlimani City, Benki ya CRDB pia inatarajia hadi ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba itazindua mashine nyengine za kisasa zaidi katika miji na sehemu zote zenye biashara kubwa kote nchini ikiwemo Mwanza, Arusha, Dodoma.
Benki ya CRDB inatajwa kuwa Benki kiongozi nchini ikiongoza katika ubunifu wa huduma na bidhaa zinazokidhi mahitaji halisi ya wateja. Benki ya CRDB inaongoza kwa kuwa na mtandao mpana zaidi wa utoaji huduma kupitia matawi zaidi ya 260, CRDB Wakala zaidi ya 22,000, ATMs zaidi ya 550, na vifaa vya manunuzi (PoS) zaidi ya 2,500.
Benki ya CRDB pia inaongoza kwa ubunifu wa mifumo ya kidijitali ya utoaji huduma ikiwamo SimBanking, SimAccount, Internet Banking, na TemboCard. Mtandao wa Benki hiyo umevuka mipaka hadi Burundi ambapo ina kampuni tanzu, na hivi karibuni inatarajia kuingia katika nchi ya Jamhuru ya Kidemokrasia ya Congo.
Mkuu wa Kitengo cha Uwakala wa Kibenki wa Benki ya CRDB, Erick Willy (wapili kulia) akiweka taarifa zake katika mashine ya kuweka pesa ( Deposit ATM) wakati wa hafla ya uzinduzi wake uliofanyika kwenye tawi ya Benki ya CRDB, Mlimani city jijini Dar es salaam.
Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Mlimani City, Zaituni Manoro akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa mashine mpya na ya kisasa ya kuweka pesa ( Deposit ATM) iliyofanyika kwenye tawi ya Benki ya CRDB, Mlimani city jijini Dar es salaam.
Social Plugin