Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati), Mkuu wa Masuluhisho ya Mikopo kwa Afrika kutoka Investec Bank, Rowan King (wapili kulia), Mkurugenzi wa Huduma za Mikopo ya Pamoja wa Benki ya Intesa Sanpaolo, Gustaaf Eerenstein (kushoto), Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Benki Kimataifa wa Bank One, Carl Chirwa (wapili kushoto) pamoja na Meneja Mikopo Maalum Benki ya Biashara ya Mauritius,Hans Dallo wakiweka mikono pamoja ikiwa ni ishara ya kuonyesha ushirikiano baada ya kusaini mikataba ya makubaliano waliyosaini inayoiwezesha Benki ya CRDB kupata kiasi cha dola za kimarekani milioni 130 kwa ajili ya kukopesha sekta za biashara na wajasiriamali nchini.
---
Benki ya CRDB leo imeingia mkataba wa makubaliano na Benki ya kimataifa ya Intesa Sanapaolo ya nchini Italia, na Investec Bank ya nchini Afrika Kusini unaoiwezesha benki hiyo kupata kiasi cha dola za kimarekani milioni 130 kwa ajili ya kukopesha sekta za biashara na wajasiriamali nchini.
Mapema mwaka huu, Benki ya CRDB iliingia mkataba wa awali na benki hizo za kimataifa kusaidia kupatikana fedha katika masoko ya kimataifa kwa ajili ya kuimarisha mtaji wa benki hiyo na kukuza uwezo wa kutoa mikopo.
“Tunafurahia sana kufanikisha makubaliano haya. Fedha hizi zilizopatikana kutoka masoko ya kimataifa zitasaidia kuimarisha mtaji wa Benki yetu na kukuza uwezo wetu wa kutoa mikopo kwa wateja wakubwa na wadogo hapa Tanzania na Burundi. Kipekee niwashukuru Investec Bank na Intesa Sanpaolo kwa ushirikiano waliotupa,” alisema Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB.
Benki ya CRDB inakuwa benki ya kwanza nchini kupata fedha za uwekezaji kutoka masoko ya kimataifa. Kwa mujibu wa Nsekela, lengo lilikuwa ni kukusanya dola milioni 50, lakini viwango bora na ufanisi mkubwa wa benki hiyo ulivutia wawekezaji wengi wa kimataifa, na kupelekea kupatikana kwa dola milioni 130.
Benki ya CRDB ni moja ya benki kumi zilizoorodheshwa kama benki bora na salama zaidi kuwekeza barani Afrika na Moody`s Investors Services na kupewa daraja la ‘B1 Outlook” ambalo ni daraja la juu zaidi kwa taasisi za fedha katika ukanda wa jangwa la Sahara. Mwaka huu Benki hiyo pia imetajwa kuwa ’Benki Bora Tanzania’ na jarida maarufu la nchini Uingereza.
“Kama Benki inayoongoza nchini Tanzania, Benki ya CRDB inaendelea kutazama fursa za biashara katika sekta za kimkakati ili kukuza uchumi wa nchi. Fedha hizi zitatusaidia kuimarisha shughuli zetu za utoaji mikopo hususani mikopo ya wanawake na vijana na kuimarisha zaidi nafasi yetu katika soko kama benki inayoongoza kwa kufadhili sekta za uchumi,” aliongeza.
Rowan King, Mkuu wa Masuluhisho ya Mikopo kwa Afrika kutoka Investec Bank, alisema kupatikana kwa fedha hizo katika masoko ya kimataifa kunaonyesha ni imani ya taasisi za fedha duniani kwa Benki ya CRDB na uchumi wa Tanzania.
"Tanzania imeonekana kuwa sehemu muhimu ya hadithi ya ukuaji wa Afrika katika miaka michache iliyopita. Bidhaa nyingi muhimu zinazozalishwa Afrika Mashariki, zinasafirishwa nje ya nchi kupitia bandari za Tanzania. Tanzania ina jukumu muhimu katika biashara katika kuimarisha biashara baina ya nchi za Afrika,” alisema.
Dola milioni 130 zilizopatikana ni mara mbili na nusu ya kiasi kilichokusudiwa, anasema Gustaaf Eerenstein, Mkurugenzi wa Huduma za Mikopo ya Pamoja Investec Bank. "Hii inaonyesha kiwango cha juu cha imani ambayo wawekezaji wanayo kwa Benki ya CRDB," alisema Eerenstein.
Ushirikiano huu na Benki ya CRDB na benki za Intesa Sanpaolo na Investec unaendelea kuimarisha uwezo wa benki hiyo katika kutoa mikopo, ambapo mwaka huu pekee imeweza kuingia makubaliano ya zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 300 na mashirika kama IFC, AFDB, AGF, PROPARCO, USAID na DFC kwa ajili ya uwezeshaji wa biashara ndogo na za kati (SME), na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake na sekta zisizo rasmi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati), Mkuu wa Masuluhisho ya Mikopo kwa Afrika kutoka Investec Bank, Rowan King (wapili kulia), Mkurugenzi wa Huduma za Mikopo ya Pamoja wa Benki ya Intesa Sanpaolo, Gustaaf Eerenstein (kushoto), Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Benki Kimataifa wa Bank One, Carl Chirwa (wapili kushoto), na Meneja Mikopo Maalum Benki ya Biashara ya Mauritius,Hans Dallo wakionyesha mikataba ya makubaliano waliyosaini inayoiwezesha Benki ya CRDB kupata kiasi cha dola za kimarekani milioni 130 kwa ajili ya kukopesha sekta za biashara na wajasiriamali nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto), Mkuu wa Masuluhisho ya Mikopo kwa Afrika kutoka Investec Bank, Rowan King (wapili kulia), Mkurugenzi wa Huduma za Mikopo ya Pamoja wa Benki ya Intesa Sanpaolo, Gustaaf Eerenstein (wapili kushoto), na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Benki Kimataifa wa Bank One, Carl Chirwa wakisaini mkataba wa makubaliano unaoiwezesha Benki ya CRDB kupata kiasi cha dola za kimarekani milioni 130 kwa ajili ya kukopesha sekta za biashara kwa wajasiriamali nchini katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es Salaam leo tarehe 15 Septemba 2022.
Social Plugin