Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DARAJA LA ESURI LALETA UKOMBOZI KWA WANANCHI OLORESHO


Wananchi wa Oloesho katika kata ya Olasiti na Olmoti, Halmashauri ya Jiji la Arusha wamepata faraja na kufurahia ujenzi wa daraja la Esuri lenye urefu wa meta 17 na upana wa meta nane (8) lililojengwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwa takribani shilingi 335,092,557.00.


Akisoma taarifa ya ujenzi wa daraja hilo kwa Bodi ya Ushauri ya TARURA wakati wa ziara ya ukaguzi, meneja wa TARURA Mkoa wa Arusha Mhandisi Laynas Sanya alisema kuwa daraja hilo lenye uwezo wa kuhimili uzito wa tani 30, litarahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi kutoka kata ya Olasiti na Olmoti na maeneo mengine ya jirani na kuondoa adha ya kutopitika kwa barabara kipindi cha mvua.


Inoti Shedrack, mkazi wa Oloresho alisema kuwa walikuwa wanateseka sana kabla ya daraja halijajegwa, hasa wakina mama na watoto lakini kwa sasa wanamshukuru Mugu daraja limekua ni mkombozi kwao.


“Tumejengewa daraja ambalo sasa hivi hatusumbuki kabisa na watoto wanaenda shule bila shida yoyote. Sisi wananchi wa Oloresho tunaishukuru sana Serikali na TARURA kwa kutengeneza daraja na barabara hii,” alisema Inoti.


Naye Mhe. Alex Martin diwani wa kata ya Olasiti alisema wanaishukuru sana TARURA kwa kutengeneza daraja hilo kwasababu walikuwa wakipata shida sana wakati wa mvua, na wakinamama wengi walikuwa wakijifungua watoto wao eneo hilo kwa wakunga wa kienyeji kutokana na kushindwa kuvuka kwenda hospitali.


“Kwa kweli tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu tumejengewa daraja hili ambalo limekuwa ni ukombozi kwetu kwa kutupunguzia adha tulizokuwa tunazipata,” alisema Alex.


Naye Mhe. Mrisho Gambo mbunge wa Arusha mjini alisema kuwa kwao imekuwa kama ndoto kwasababu walizoea kuona TANROAD ndiyo wanaweza kujenga madaraja yenye viwango bora kama hilo.
“Tumeona kuwa kumbe TARURA ikiwezeshwa inaweza kufanya mambo makubwa zaidi na kuwafikia wananchi wengi zaidi. Tunaishukuru sana bodi yako mwenyekiti; mtendaji mkuu pamoja na watumishi wa TARURA ambao wametoa ushirikiano mkubwa sana kukamilika kwa daraja hili. Niwasihi madiwani wangu tuendelee kuiamini TARURA na wataendelea kufanya mambo makubwa tukiwaunga mkono,” alisema Mhe. Gambo.


Kwa upande wake Mhandisi Florian Kabaka, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA aliwashukuru wananchi pamoja na mbunge kwa kutambua na kuona kazi ambayo TARURA inafanya ya kuwahudumia wananchi na kurahisisha utoaji huduma kupitia barabara.


“Nimefarijika sana kuona daraja hili limewanufaisha sana sasa watu hawachukui muda mrefu sana kama zamani, wanaweza kukatisha hapa na kufika wanapotaka kwenda kwa urahisi na kupata huduma zao, na hili ndilo lengo la TARURA,”alisema Mhandisi Kabaka.


Aidha aliwashukuru wananchi kwa kutambua kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda na kuwajali kwa kuwawezesha TARURA kuwafikia na akaahidi kuwa TARURA itaendelea kuboresha zaidi kadiri inavyowezeshwa.


Mhandisi Victor Seff, Mtendaji Mkuu wa TARURA aliwaasa viongozi na wananchi wa eneo hilo kuilinda miundo mbinu hiyo na hasa alama za usalama zilizowekwa ili ziwanufaishe wao pamoja na vizazi vijavyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com