Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda
Na Dotto Kwilasa, DODOMA.
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewataka wadau wa elimu nchini wanaoshiriki katika kikao maalum cha Menejiment ya wizara na wadau wa elimu kutoa maoni ya kuboresha sera na mitaala ya Elimu ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sekta hiyo muhimu Duniani.
Waziri mwenye dhamana ya Elimu nchini Prof. Adolf Mkenda amesema hayo wakati akizungumza leo jijini Dodoma na kusema kuwa kikao hicho ni kutekeleza Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani.
Amefafanua kuwa agizo hilo alilitoa Mnamo Tarehe 22 Aprili 2022 Bungeni ambapo alitaka kufanyike marekebisho ya sera ya Elimu ya mwaka 2014 pamoja na mitaala iliyopo kwa maslahi ya Taifa na Watu wake.
Prof. Mkenda amesema kuwa huwezi kuzungumzia ubora wa elimu bila kufanya mageuzi na mabadiliko katika sera na mitaala ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Dunia kwani kwa sasa taaluma na ujuzi zinakwenda sambamba.
"Tunapokwenda kufanya mageuzi ya elimu ni lazima twende na adhma ya Mhe. Rais aliyeagiza kuwa mbali tu na kujikita katika elimu ya taaluma tujikite pia katika Ujuzi hivyo ni lazima tuhakikishe tunatoa mawazo ambayo itasaidia kuboresha elimu yetu sio kushusha ubora,"amesema Prof. Mkenda.
Na kuongeza kuwa "Suala la elimu sio la Tanzania peke yake ni la kidunia hivyo lazima tufanye mageuzi ili kuendani na kasi ya mabadiliko katika sekta ya elimu duniani,"amesema.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Abdugulam Hussein amesema vijana lazima waandaliwe kitalamu na kiubunifu ili waweze kulitetea Taifa kimaendeleo na kushindana kimasoko.
Pia Mhe. Ali Abdugulam Hussein amesema kuwa swala la sera na mitaala ya elimu ndio kila kitu katika maboresho ya elimu hivyo kukifanyika makosa katika mapitiao haya yanaweza kulipoteza taifa.
"Sera na mitaala ni vyanzo muhimu katika elimu ya nchi yeyote duniani hivyo niwaombe washiriki wa kikao hiki maalum mtoe mawazo huku mkijua kuwa michango yenu ndio itakayokuja na sera na mitaala madhubuti,"amesema Mhe. Ali Abdugulam Hussein.
Dhima ya sera mpya na mitaala ya Elimu nchini ni kuinua ubora wa Elimu na Mafunzo na Kuweka Mifumo na Taratibu zitakazowezesha Kupata idadi Kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikisha Malengo ya Maendeleo ya Taifa.