Wanafunzi pamoja na wakazi wa sofu wakipokea maelekezo ikiwemo sala na dua iliyofanyika shuleni hapo.
Na Daniel Limbe, Kibaha
WANAFUNZI waliosajiliwa kujiunga na shule ya sekondari Sofu iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani wanatarajiwa kunufaika na mchepuo mpya wa masomo ya Kichina.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa shule hiyo,Kharima Yusuph, wakati akizungumza na mwandishi wetu aliyetaka kujua uwepo wa shule mpya ya Koka itakavyowanufaisha wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kwenda kusoma kwenye shule ya sekondari Nyumbu pamoja na Picha ya Ndege.
Mbali na kuipongeza serikali pamoja na jamii ya wananchi wa kata ya Sofu, ameomba kuwepo kwa muunganiko kati ya walimu wazazi na wanafunzi iwapo jamii hiyo inahitaji kupata mabadiliko ya haraka kitaaluma.
"Tunaipongeza sana serikali yetu kwa kuwa imetupatia walimu 18 wa masomo yote na kwamba shule yetu itaanza pia kufundishia somo la kichina...pia tumefanikiwa kuanza na wanafunzi 58,madarasa sita,choo cha kiume na cha kike vikiwa ni vya kisasa kabisa kama unavyojionea mwenyewe", amesema.
Ofisa elimu Kata ya sofu,Jane Tenga, ameahidi kusimamia kikamilifu taaluma ili kuhakikisha shule hiyo inakuwa miongoni mwa shule bora katika wilaya ya Kibaha na mkoa wa Pwani kwa ujumla.
"Ninakuahidi mtihani wa kidato cha pili mwakani utaona maajabu ya ufaulu wa shule hii...hatuna sababu ya kushindwa wakati wanafunzi watakaa 30 kwa kila darasa...akidi hii itamsaidia kila mwalimu kumtambua mtoto mwenye uzito wa kupokea na namna ya kumsaidia",amesema.
Mtendaji wa kata hiyo, Saumu Hassan, amepongeza jitihada zilizoonyeshwa na wananchi wa kata hiyo kwa kujitolea kuchimba msingi,kuchangia fedha pamoja na mawazo yao kwa lengo la kufanikisha ujenzi wa shule hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Kibaha,Mussa Ndomba,ametumia fursa hiyo kuwataka wanafunzi waliosajiliwa kwenye shule hiyo kusoma kwa bidii ili kitimiza malengo yao badala ya kujihusisha katika makundi yasiyofaa ikiwemo uvutaji wa bangi.
Sambamba na hilo,amesema halmashauri yake inakusudia kuendelea na ujenzi wa miundombinu mingine kwenye shule hiyo katika bajeti ya mwaka 2022/23 ikiwemo vyumba vinne vya madarasa na ujenzi wa maabara ya kisasa.
Social Plugin