Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Sinde jijini Mbeya, Faraja Kasole (16), ameuawa kwa kukatwa na shoka shingoni na mwanafunzi mwenzie aitwaye Humphrey Ngogo (17) mwanafunzi wa kidato cha tano shule ya sekondari Iduda, baada ya kushindwa kumbaka.
Chanzo cha mauaji hayo kimedaiwa kuwa ni tamaa za kimwili ambapo mtuhumiwa Ngogo alifanya jaribio la kumbaka marehemu, lakini baada ya kuzidiwa nguvu akachukua shoka na kumpiga nalo kichwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urilich Matei amesema tukio hilo limetokea Septemba 4, 2022 na kwamba marehemu alikuwa mwanafunzi kidato cha nne Shule ya Sekondari Sinde.
Amesema kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa alifika nyumbani kwa marehemu ambaye kwa muda huo alikuwa peke yake na kisha kumvamia chumbani kwake kwa nia ya kumbaka na alipozidiwa nguvu ndipo aliamua kuchukua shoka na kumpiga nalo.
''Baada ya purukushani na marehemu kumzidi nguvu mtuhumiwa ndipo alipochukua shoka lililokuwepo katika nyumba hiyo na kisha kumkata kichwani na kusababisha kifo chake baada ya kuvuja damu nyingi,'' amesema.
Amesema tayari Jeshi la Polisi linamshikilia Humphrey Humphrey (17) na kwamba mtuhumiwa huyo alipohojiwa na Polisi amekiri kuhusiana na tukio hilo na atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mjomba wa marehemu Faraja Kasole, aitwaye, Sauli Mwaisenye, amesema maziko yalifanyika Septemba 4 mwaka huu katika makaburi ya Iyela jijini Mbeya, na kwamba familia inaomba vyombo vya maamuzi kutenda haki.