Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa George Chiteto amefariki dunia jana mchana mara baada ya kumaliza kuhubiri katika mazishi ya mke wa Askofu Lugendo wa Dayosisi ya Mbeya Bi. Hilda Lugendo yaliyofanyika wilayani Muheza mkoani Tanga.
Tukio hilo la huzuni limekuja ghafla mara baada ya kumaliza mahubiri katika msiba huo, Askofu George Chiteto alirudi kukaa kwenye kiti ili taratibu zingine za ibada ziendelee, alianza kujisikia vibaya, akaishiwa nguvu kisha kupoteza fahamu.
Utaratibu wa kumkimbiza hospitali ulifanyika haraka na kufikishwa katika hospitali teule ya wilaya ya Muheza Tanga na saa chache akaaga dunia.
Askofu George aliwekwa wakfu Jumapili iliyopita Agosti 28, 2022 kuwa Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa iliyopo wilaya ya Mpwapwa jijini Dodoma na Septemba 03, 2022 akawa ameaga dunia akihudumu nafasi hiyo ya uaskofu wa Dayosisi hiyo kwa takribani siku kati ya tano tu.
Askofu mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, aliyekuwepo katika ibada hiyo ya mazishi jijini Tanga, ndie aliyetangaza msiba huo uliolikumba kanisa hilo.
Katika mahubiri ya leo na ya mwisho Marehemu Askofu George Chiteto amehubiri ujumbe unaosema "JITAHIDI UINGIE KATIKA ULE MJI MTAKATIFU" ambapo alitolea mfano ya kuwa, hata yeye angetamani kifo cha amani.
Askofu Chiteto alipata Ushemasi mwaka 1987 na Daraja la Ukasisi mwaka 1988, ana Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Theolojia (Masters of Arts in Theology) kutoka Chuo Kikuu cha St. John’s - Dodoma aliyoipata mwaka 2012.
Social Plugin