Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa akikabidhi kombe kwa Timu ya Kewanja FC iliyotwaa ubingwa wa Mashindano ya Soka ya Kombe la Mahusiano 2022 yaliyoandaliwa na Barrick North Mara. Wa pili kutoka kulia ni Menaja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko na Katibu wa Mbunge wa Tarime Vijijini, Remmy Mkapa (kulia).
Wachezaji wa Timu ya Kewanja FC wakifurahia ushindi
Wachezaji wa timu za Kewanja FC na Murito FC wakimenyana katika mechi ya fainali
Viongozi wa Serikali na Barrick North Mara wakigawa medali kwa wachezaji wa Murito FC iliyoshika nafasi ya pili kwenye Mashindano ya Kombe la Mahusiano 2022.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa akikabidhi zawadi ya mpira kwa mchezaji bora wa Mashindano hayo.
Wachezaji wa Kewanja FC (kushoto) wakishangilia ubingwa
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko (aliyesimama) akizungumza wakati wa fainali ya Mashindano hayo.
Katibu wa Mbunge wa Tarime Vijijini, Remmy Mkapa (wa pili kutoka kushoto) na viongozi wa Idara ya Mahusiano wa Barrick North Mara wakifurahia jambo wakati wa fainali ya Mashindano hayo.
***
TIMU ya Kewanja FC imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Soka ya Kombe la Mahusiano “Mahusiano Cup” baada ya kuichapa Murito FC bao 1-0 katika mchezo wa fainali.
Fainali hiyo ilichezwa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Ingwe mjini Nyamongo wilayani Tarime na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara ambayo imeandaa na kudhamini mashindano hayo.
Mgeni rasmi alikuwa ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa alishirikiana na Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko ambao mbali na kutoa kombe la ushindi kwa Kewanja FC, pia walikabidhi zawadi ya fedha taslimu shilingi milioni 1.5.
Murito FC ilipewa zawadi ya Shilingi milioni moja kwa kuingia fainali na kushika nafasi ya pili katika mashindano hayo ambayo yalishirikisha timu 16 kutoka vijiji mbalimbali vya Halmshauri ya Wilaya ya Tarime.
Vijiji hivyo vilivyoshiriki mashindano hayo ni Genkuru, Msege, Komarera, Nyamwaga, Kewanja, Nyakunguru, Kerende, Nyabichune, Mjini Kati, Matongo, Nyangoto, Mrito, Keisangora na Nyarwana.
Mashindano ya Kombe la Mahusiano yalizinduliwa Septemba 14, mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele kwa kushirikiana na Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko, miongoni mwa viongozi wengine.
Mashindano hayo yaliandaliwa na Kampuni ya Barrick North Mara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, yakiwa na kaulimbiu inayosema “Mahusiano Bora kwa Uwekezaji Endelevu.” Na yamelenga kukuza uhusiano mzuri kati ya Mgodi na jamii inayozuguka mgodi huo.
Aidha, mashindano hayo yamesaidia kuongeza uelewa juu ya fursa mbalimbali zilizopo na kushughulikia masuala mtambuka, hasa uvamizi, uharibifu wa miundombinu (vandalism) na utegeshaji wa mazao, miti na nyumba.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko alisema michezo ni nyenzo muhimu ya katika kujenga na kudumisha mahusiano.
Mkuu wa Wilaya, Kanali Mntenjele aliwataka washiriki wa mashindano hayo kucheza kwa amani na wasimamizi husika kutenda haki bila kupendelea timu yoyote.
Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliipongeza Barrick North Mara, kwa kuandaa mashindano hayo, akisema yatahamasisha ushirikiano kutoka kwa jamii inayozunguka mgodi huo ili kuwezesha kila upande kunufaika.
Uzinduzi wa mashindano ya soka ya Mahusiano Cup pia ulitanguliwa na michezo mbalimbali ikiwemo ya kuvuta kamba, kufukuza kuku na ngoma ya asili, kabla ya timu za Kewanja FC na Mosege FC kucheza mechi ya ufunguzi.
Social Plugin