TAARIFA KWA UMMA
MATUKIO YA MAUAJI YANAYOENDELEA NCHINI NA KULETA HOFU KWA JAMII
Septemba 15, 2022
Chama Cha Waandishi wa Habari za Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (OJADACT) kinalaani mwenendo wa matukio ya mauaji yanayoendelea kwenye jamii na kusababisha hofu kwa jamii pamoja na kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
OJADACT inasikitika kuona matukio hayo yakiendelea kutokea na kuchafua taswira ya Taifa kwenye kulinda amani na usalama wa raia wake pamoja na kutumia rasilimali nyingi za Taifa kwenye kupambana na vitendo vya kihalifu.
Baadhi ya matukio yaliyotokea ni tukio la Septemba 14, 2022, la mauaji ya Mwanafunzi wa Chuo Kikuu, Maria Bosco lililotokea eneo la Kawe Mzimuni, Jijini Dar es salaam lililofanywa na vijana zaidi ya thelathini ambao walitekeleza mauaji , kujeruhi na kupora vitu mbalimbali vikiwemo simu na fedha.
Tukio jingine, tukio la mauaji ya watu wanne lililotokea Jijini Mbeya ambapo Mwalimu wa Shule ya Msingi Bwana Saimon Mtambo (44) alimkata mapanga mke wake na watoto wake wawili na kisha yeye kunywa sumu na kupoteza Maisha.
Tukio jingine, tukio lililotekea Mkoa wa Mtwara, ambapo Kijana Kristatus Victory (23) Mkazi wa Lukuledi Wilaya ya Masasi anatuhumiwa kumuua Baba yake Mzazi Victory Milanzi (74)kwa madai ya kushindwa kumtafutia mchumba wa kuoa.
Tukio jingine, tukio la Mkazi wa Kihesa Kilolo Mkoani Iringa Enea Mkimbo (55) aliyefariki Dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kitenge kwa madai ya kuzongwa na madeni ya vikoba.
OJADACT imebainisha matukio haya Machache ikiwa ni sehemu tu ya matukio yanayoendelea kwenye jamii, matukio hayo yamekuwa yakisabishwa na sababu mbalimbali ikiwemo, tamaa za kujipatia fedha, wivu wa kimapenzi, mmomonyoko wa maadili , hali ngumu ya maisha na ushirikina na mani potofu kwenye jamii.
OJADACT inatoa mapendekezo yafuatayo.
1. Kuundwa kwa mkakati wa kitaifa wa kuzuia uhalifu ili kusaidia kupunguza matukio haya ya mauaji na uhalifu mwingine kwa kuwaleta wadau pamoja na kuweka mikakati mahususi.
2. Kuimarisha maadili ndani ya jamii ili kuwa na jamii yenye kuheshimu utu na ubinadamu.
3. Serikali kupitia taasisi zake za kupambana na uhalifu pamoja na ustawi wa jamii kufanya tafiti za kutosha ili kugundua chanzo cha mauaji na uhalifu Nchini.
4. Jeshi la Polisi kuongeza kasi ya kupambana na matukio ya kihalifu hasa vikundi visivyo rasmi vinavyofanya uhalifu.
5. Vyombo vya habari na taasisi za kihabari kutengeneza maudhui yenye kuhamasisha watu kutofanya uhalifu Zaidi kuliko kuripoti matukio ya kihalifu Zaidi.
*Edwin Soko*
*Mwenyekiti*
*OJADACT*
*15.09.2022*