MKUTANO mkuu wa Chama cha NCCR Mageuzi umemtimua uanachama aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho Taifa, James Mbatia na kumvua uongozi Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Angelina Rutairwa.
Aidha, mkutano huo ulitaka viongozi wote waliohusika na ubadhilifu wa mali akiwemo Mbatia kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mkutano huo unafanyika leo Jumamosi Septemba 24, 2022 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wajumbe 224 kati ya 368 waliopo kwa mujibu wa Katiba ya chama chao.
Wajumbe hao walifanya hivyo baada ya Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Haji Ambari Hassan kutaja tuhuma saba zinazomkabili Mbatia na tuhuma mbili za Angelina.
Miongoni mwa tuhuma hizo Mbatia ni kuuza mali za chama, ikiwemo mashamba na nyumba katika maeneo mbalimbali.
Ambari amewaambia wajumbe hao kuwa viongozi hao walipelekewa hati ya mashtaka yao na walitakiwa kujibu ndani ya siku 14 kama katiba yao inavyotaka.
Social Plugin