Mwanamke aitwaye Hadija Abdallah Magomba (25), mkazi wa Kijiji cha Mchakama, wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, ameteguka kiuno, nyonga na mkono baada ya kuanguka kutoka juu ya mnazi akidaiwa kufanya jaribio la wizi wa nazi.
Taarifa iliyothibitishwa na mamlaka ya serikali ya Kijiji hicho, pamoja na mmiliki wa shamba linalodaiwa kuibwa nazi hizo, zinaeleza wizi huo unadaiwa kufanywa na mwanamke huyo Septemba 14 mwaka huu, saa 7:00 usiku.
Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Mkwepu Ally Mkwepu na Mwenyekiti wake, Mohamedi Mpinga na mmiliki wa shamba Jonas Timothew, wamekiri kutokea kwa tukio hilo,na kueleza mwanamke huyo amepatwa na anguko hilo alipopanda juu ya mnazi akijaribu kuiba nazi.
Mkwepu alisema siku hiyo muda wa saa 7:00 usiku akiwa nyumbani kwake amelala usingizi alipigiwa simu na Mwenyekiti wa Kijiji hicho akimuagiza kumpatia Hadija Magomba barua ya kwenda kupata huduma ya matibabu kwenye Zahanati,jambo ambalo amelitekeleza.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mohamedi Mpinga, amesema siku hiyo Hadija Magomba, akidaiwa kuwa na mpenzi wake wa kiume aliyemtaja kwa jina la Hassan Kongaya walikwenda shambani kwa Timothew kujaribu kuiba nazi.
Amesema baada ya kupanda juu ya mnazi unaokaribia kuwa na urefu usiopungua zaidi ya mita 50, huku mshirika wake ambaye anadaiwa ni mpenzi wake waliobahatika kupata mtoto mmoja, alibaki chini akisubiri kuokota nazi zilizokuwa zinadondoshwa na mwanamke huyo.
Mpinga amsema wakati nazi hizo zikidondoka juu ya mti, walinzi wa shamba walitoka nje ili kutaka kufahamu kinachoendelea kutokea huko nje na ndipo mwanamke huyo alijiachia kutoka juu ya mnazi alioupanda kisha kudondoka chini na kusababisha nyonga, kiuno na mkono wa kushoto kupata athari ya kuumia, huku mshirika aliyekuwa naye akitimua mbio.
Chanzo- EATV
Social Plugin