Picha haihusiani na habari hapa chini
Mapuli Misalaba, Shinyanga
Mkazi wa mtaa wa Mwabundu kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga Charles Mayunga (38) amelazwa katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga baada ya kujeruhiwa na kitu chenye makali kichwani na usoni akiwa kwenye klabu cha Pombe kata ya Ngokolo.
Tukio hilo limetokea Septemba 4,2022 majira ya saa sita mchana kata ya Ngokolo mjini Shinyanga.
Misalaba Blog imefika katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga na kuzungumza na majeruhi huyo ambaye ameeleza kuwa alifika kwenye klabu cha Pombe akaweka fedha mezani shilingi elfu kumi na nane akaendelea kunywa ambapo inasadikika watuhumiwa hao walizitamani fedha hizo baada ya kukataa kuwanunulia Pombe.
Mayunga amesema kuwa aliendelea kunywa Pombe baada ya muda mfupi akaanza kushambuliwa hali iliyopelekea kupata majeraha kichwani na usoni.
“Nilitoka nyumbani nikaenda Ngokolo nikafika kwa muuza Pombe mmoja anaitwa Kofi wakati nimeagiza pale Pombe kumbe wale watu niliokuwa nao pembeni hela zangu wamezitamani mimi nikaendelea kunywa baada ya muda nikashangaa tu napigwa Panga nikaanguka nikapoteza fahamu”.
“Nilikuja nikiwa na hali mbaya sana yaani nilikuwa nikikaa najisikia kizunguzungu halafu na damu zilikuwa zikitoka kwa wingi ila namshukuru sana Dokta alivyokuja alinishughulikia hakuangalia sina hela wala nini mpaka sasa naona hali yangu ni nzuri”. Amesema Mayunga
Kwa upande wake mkuu wa idara ya kitengo cha upasuaji katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Kambi Athuman Buteta amekiri kumpokea mgonjwa huyo siku ya jana akiwa na hali mbaya na kwamba baada ya kumpa huduma stahiki hali yake inaendelea vizuri.
“Tulimpokea akiwa amepata majeraha kichwani ya kupigwa na kitu chenye ncha kali alikuwa anatokwa na damu nyingi kichwani na tulimpatia huduma ya kwanza pamoja na kumsafisha na kumshona vizuri sasahivi anaendelea na matibabu na hali yake ni nzuri”.amesema Dkt, Kambi
Aidha kamanda wa jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi polisi Janeth Magomi amesema bado hajapokea taarifa za tukio hilo.
CHANZO - Misalaba blog
Social Plugin