Mahakama ya juu imeidhinisha Uchaguzi wa William Ruto kuwa rais mteule wa Kenya baada ya kesi iliowasilishwa na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo Raila Odinga kukosa ushahidi wa kutosha.
Wakitoa uamuzi wao wa pamoja, majaji hao walioongozwa na jaji mkuu Martha Koome walisema kwamba ushahidi uliotolewa na mlalamishi Raila Odinga ulikuwa umejaa uvumi na porojo.
Akiangazia maswala tisa ya kesi hiyo, Jaji Martha Koome amesema kuwa mshindi wa uchaguzi huo William Ruto alifanikiwa kupita kikwazo cha kura asilimia 50 na moja ya kikatiba.
Akitangaza matokeo hayo , mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati, alimtangaza Dkt Ruto kuwa Rais mteule baada ya kupata kura milioni 7,176,141 (asilimia 50.49) dhidi ya milioni 6,942,930 za Bw Odinga (asilimia 48.85) )Prof George Wajackoyah wa Roots Party alifanikiwa kura 61,969 (asilimia 0.44) huku David Mwaure Waihiga wa Agano Party akiibuka wa nne kwa kura 31,987 (asilimia 0.23).
lakini akitoa uamuzi huo jaji mkuu Martha Koome alisema kwamba kura zilizokataliwa haziwezi kujumlishwa katika hesabu ya kumtafuta aliyeibuka mshindi.
Bi Koome alisema kwamba mbinu iliotumika na tume ya uchaguzi kupata asilimia 64.4 ya wapiga kura ilikuwa sahihi.
Mzozo juu ya nani alikuwa na uwezo wa kusoma matokeo
Kuhusu ni nani aliyekuwa na uwezo wa kujumlisha na kuthibitisha matokeo katika tume ya uchaguzi ya IEBC , jaji wa Mahakama ya Juualisema kwamba mamlaka ya kuthibitisha na kujumlisha matokeo ya uchaguzi wa urais hayatokani na mwenyekiti bali tume.
Alisema kwamba Sambamba na maamuzi ya awali ya mahakama - mwenyekiti hawezi kujipa mamlaka ya kuthibitisha na kujumlisha matokeo bila kuwajumuisha wengine.
Hatahivyo majaji walizingatia ukweli kwamba makamishna wanne waliopinga matokeo ya mwisho walishiriki katika uhakiki wa awali na kujumlisha matokeo.
BI Koome alisema kwamba makamishna hao wanne hawakutoa hati yoyote inayoonyesha matokeo yalibadilishwa na hawakueleza ni kwa nini walishiriki katika mchakato wa uhakiki ambao walisema "haukuwa wazi",.
Madai ya kuingiliwa kwa mfumo wa teknolojia wa IEBC
Wakiangazia suala la kuingiliwa kwa tovuti ya matokeo,majaji hao wamesema kwamba hakuna ushahidi kwamba mfumo wa matokeo uliingiliwa.
Bi Martha , alisema kwamba hakukuwa na ushahidi kwamba mtu yeyote aliingilia mfumo wa utumaji matokeo kwa lengo la kuvuruga matokeo.
Aliongezea kwamba tume ilieleza vya kutosha jinsi mfumo ulivyonasa fomu za matokeo zilizowekwa katika tovuti yake na kwamba zote zilikuwa sawa na zile zilizowasilishwa katika kituo kikuu cha kuhesabia kura.
Social Plugin