Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MARAIS 20 KUSHUHUDIA WILLIAM RUTO AKIAPISHWA LEO...TAYARI SAMIA AMEWASILI


RAIS mteule wa Kenya William Ruto leo anachukua hatamu za uongozi pindi tu atakapoapishwa katika sherehe kubwa inayofanyika jijini Nairobi.


Zaidi ya marais 20 na wakuu wa nchi wanatarajiwa kushuhudia rais anayeondoka Uhuru Kenyatta akikabidhi madaraka kwa naibu wake huku watu takriban 60000 wakitarajiwa kushuhudia hafla hiyo wakati Kenyatta atakapomkabidhi mrithi wake vyombo vya mamlaka ikiwa ni pamoja na upanga na nakala ya Katiba.

Rais Kenyatta jana alikutana na Ruto katika ikulu ya Nairobi na kumpongeza kwa mara ya kwanza hadharani kwa ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 huku akimtakia kila la heri .


Kwenye hotuba yake, alirejelea miradi ya maendeleo aliyotekeleza katika utawala wake wa mihula miwili.

Uchaguzi wa Ruto kama Rais wa tano wa Kenya uliidhinishwa na Mahakama ya Juu, ambayo ilitupilia mbali ombi la uchaguzi lililowasilishwa na mgombea urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga ambaye alidai ushindi wake umeibiwa na kutaka kutangazwa mshindi.


Odinga kutohudhuria

Kiongozi wa muungano wa Azimio La Umoja Raila Odinga jana alisema hatahudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais mteule William Ruto .

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, Odinga alikiri kuwa Ruto alimwalika yeye binafsi kwenye hafla ya kuapishwa kwake lakini akasema hataheshimu mwaliko huo kwa vile yuko nje ya nchi na kwamba bado ana wasiwasi mkubwa kuhusu uchaguzi wa Agosti 9 ambao Ruto alitangazwa mshindi.


Odinga alikariri msimamo wake wa awali kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haikuendesha uchaguzi huru na wa haki.

Katika taarifa hiyo, Odinga aliendelea kushikilia kuwa anaamini kuwa uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi uliothibitisha kuchaguliwa kwa Ruto “haukuegemea ukweli na sheria, ingawa tuliukubali.”


 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com