Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GGML WAZINDUA MASHINDANO YA SOKA KWA WATOTO WANAOZUNGUKA MGODI

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited, Terry Strong akisalimiana na timu ya soka ya watoto wanaozunguka kampuni hiyo kutoka Kata za Mtakuja na Nyankumbu zilizopo mkoani Geita. GGML jana imezindua mashindano ya mpira wa miguu kwa watoto hao ili kukabiliana na changamoto ya watoto wanaokwepa kwenda shule na kuingia kwenye eneo la mgodi na kufanya shughuli za uchimbaji bila ruhusa.
Waliosimama kutoka kulia ni Mratibu wa Miradi inayofadhiliwa na GGML kupitia mpango wa Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR), Moses Rusasa; Makamu Rais wa AngloGold Ashant-GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo; Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong; Afisa Tawala wa mkoa wa Geita, Janeth Jonathan na wageni wengine wakiwa katika picha ya pamoja na timu ya soka ya watoto wanaozunguka mgodi wa GGML.
Waliosimama kutoka kulia ni Mratibu wa Miradi inayofadhiliwa na GGML kupitia mpango wa Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR), Moses Rusasa; Makamu Rais wa AngloGold Ashant-GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo; Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong; Afisa Tawala wa mkoa wa Geita, Janeth Jonathan na wageni wengine wakiwa katika picha ya pamoja na timu ya soka ya watoto wanaozunguka mgodi wa GGML.


Na Mwandishi Wetu - Geita

KAMPUNI ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu Geita (GGML) imezindua mashindano ya mpira wa miguu kwa watoto wanaozunguka mgodi huo ili kukabiliana na changamoto ya watoto kuingia kwenye eneo la mgodi na kufanya shughuli za uchimbaji bila ruhusa.

Mashindano hayo yanayohusisha kata za Mtakuja na Nyankumbu za Geita Mjini, yanalenga kuwapatia elimu watoto, walezi na wazazi wao madhara ya kuwatumikisha watoto wadogo katika shughuli za uchimbaji na kuwanyima fursa za kupata elimu.

Katika mashindano hayo, watoto kutoka mtaa wa Nyamalembo na Compound walimenyana na watoto kutoka mtaa wa Elimu na Nyankumbu.

Aidha, akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika uwanja wa General Tyre mjini Geita jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited, Terry Strong alisema watoto ni sehemu muhimu katika biashara ya kampuni hiyo.

Alisema GGML imewekeza kwenye shule, hospitali na maeneo mengine ambayo watu wanaweza kupata huduma... ikiwa ni sehemu ya Wajibu wa Kampuni kuisadia Jamii inayozunguka mgodi ambapo kupitia mpango huo, GGML ilijenga zaidi ya madarasa 600 mwaka wa 2018.

“Watoto wadogo ndiyo kizazi cha baadaye na ndiyo wa kwanza kunufaika na uwekezaji wetu. Kampuni yetu inafuata kanuni Elekezi za Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Kibinadamu na Kanuni za Hiari za Usalama na Haki za Kibinadamu (VPSHR) (UNGP).

“Kwa hivyo, tumekubali kuwalinda watoto dhidi ya hatari zozote zinazotokana na jinsi tunavyofanya biashara,” alisema.

Alisema idadi ya watoto wanaoingia kwenye shughuli za uchimbaji bila ruhusa imekuwa ya kutisha.

“Kwa kawaida sisi hutumia neno "kuwaokoa watoto" badala ya "kuvamia mgodi " kwa sababu watoto wapo chini ya umri wa watu wazima na wanalindwa na sheria za kitaifa na kimataifa.

“Hata hivyo, kutokana na ufuatiliaji wetu ni kwamba watoto wengi waliookolewa baada ya kuingia kwenye eneo la machimbo bila ruhusa, wengi wao tumekuwa tukiwakuta ndani au nje ya leseni yetu ya uchimbaji,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa takwimu walizonazo ni kwamba watoto 680 waliokolewa ndani na nje ya eneo la shughuli za mgodi katika mgodi wa GGML kati ya mwaka 2019 na 2020.

Alisema ili kukabiliana na hili, GGML imekuwa ikishirikiana na serikali za mitaa kuzindua mfululizo wa kampeni za uhamasishaji, ikijumuisha ushirikiano wa moja kwa moja na shule za sekondari na msingi.

Aliongeza kuwa katika juhudi za kuwachangamsha watoto, kuwahusisha na michezo na kuwajengea mtindo bora maisha kwa manufaa ya afya zao, tumeamua kuandaa mashindano ya watoto katika kipindi cha likizo katika hali ya uchangamfu na kwenye kipindi chao cha likizo,

“Tunatarajia kuwa vijana wenye vipaji wataibuka kila mwisho wa shindano, na kwamba wataajiriwa na vilabu vikubwa kama Geita Gold Football Club (inayodhaminiwa na GGML) ili kuzidi kuonesha uwezo wao katika uwanja wa Magogo (pia unaodhaminiwa na GGML). Mpango ni kuwaokoa watoto hawa na kuwasaidia kukuza vipaji vyao,” alisema.

Awali, Makamu wa Rais wa AngloGold- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa Ghana na Tanzania, Simon Shayo alisema moja ya tunu muhimu za kampuni hiyo ni kuhakikisha jamii inayozunguka mgodi huo inanufaika.

Alisema mipango ya kampuni hiyo inalenga kuboresha sekta ya afya, elimu, michezo na utamaduni ili kukuza vipaji vya watoto hao.

Aidha, Afisa utawala wa mkoa wa Geita, Janeth Jonathan akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo, alisema wazo la kuanzisha mashindano hayo lilitokana na kamati iliyoundwa ili kukabiliana na wimbi la watoto wanaofanya kazi hatarishi katika eneo la Nyamatagata lenye mlipuko wa madini.

Alisema licha ya kwamba GGML imejenga uwanja, michezo kwa watoto inatakiwa kuzingatiwa ili kuwaondoa katika wimbi hilo la ajira hatarishi hasa ikizingatiwa watoto wanahusishwa zaidi kuchenjua madini kazi ambayo inahusisha kushika kemikali hatari za mercury.

Naye Afisa Kazi kutoka idara ya kazi mkoani humo, Jofrey Oled alitoa wito kwa wazazi kuacha watoto wapate muda wa kusoma badala ya kuwatumikisha kwenye kazi hatari kwani ni kosa kisheria.

Alisem kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano kazini, mzazi atakayepatikana na kosa hilo atapata adhabu ya kulipa faini Sh milioni tani au kwenda kutumia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote viwili.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com