Sokwe mwitu wana "mtindo wao wa kupiga ngoma " kwa mujibu wa wanasayansi.
Watafiti waliofuatilia na kuchunguza sokwe katika msitu wa Uganda waligundua kuwa wanyama hao hutumiana ujumbe wao kwa wao kwenye mizizi ya miti.
Wanasayansi hao wanasema kwamba ishara ya midundo huwaruhusu kutuma taarifa kwa umbali mrefu, kufichua ni nani yuko wapi na anafanya nini.
Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la wanyama la Animal Behaviour.
Dkt Catherine Hobaiter kutoka Chuo Kikuu cha St Andrews alieleza kuwa nyani hao wa porini hutumia mizizi mikubwa ya miti kama ubao ili kupiga ngoma kwa mikono na miguu.
"Ukigonga mizizi kwa nguvu sana, inasikika na kutoa sauti kubwa ya kina, inayovuma ambayo husafiri msituni," aliambia kipindi cha Sayansi ya BBC Radio 4.
"Mara nyingi tuliweza kutambua ni nani aliyekuwa akipiga ngoma tulipowasikia; ilikuwa ni njia nzuri sana ya kuwapata sokwe mbalimbali tuliokuwa tukiwatafuta. Kwa hiyo kama tumeweza kufanya hivyo, tulikuwa na uhakika wangeweza pia."
Kila sokwe dume, wanasayansi waligundua, hutumia muundo tofauti wa mapigo. Wanaichanganya na sauti za masafa marefu, zinazoitwa pant-hoots. Na wanyama tofauti hupiga ngoma katika sehemu tofauti.
Mtafiti mkuu juu ya utafiti huu, mwanafunzi wa PhD Vesta Eleuteri kutoka Chuo Kikuu cha Vienna, alielezea jinsi baadhi ya viumbe kuwa na mdundo wa mara kwa mara, kama wapiga ngoma za rock na blues, ilhali wengine wana midundo tofauti zaidi, kama jazz.
"Nilishangaa kwamba niliweza kutambua ni nani aliyekuwa akipiga ngoma baada ya wiki chache tu msituni," alisema. "Lakini midundo yao ya ngoma ni ya kipekee sana kwamba ni rahisi kuipokea."
CHANZO-BBC SWAHILI
Social Plugin