***
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa semina elekezi kwa wafanyabiashara wanaoagiza na kuuza bidhaa mbalimbali za chakula na vipodozi jijini Mwanza ili kuwajengea uwezo kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia Sheria.
Semina hiyo imefanyika Alhamisi Septemba 29, 2022 ikiwashirikisha wafanyabishara mbalimbali wakiwemo waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, wamiliki wa maghala ya kuhifadhia bidhaa na wamiliki wa maduka makubwa ya bidhaa za jumla.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya Nyamagana mkoani Mwanza Amina Makilagi aliwataka wafanyabishara kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanaingiza nchini bidhaa zenye ubora zisizo na madhara kwa watumiaji
Alisema Mwanza ni jiji la pili kiuchumi nchini na pia kitovu cha biashara katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki hivyo ni vyema wafanyabishara wakatumia fursa hiyo vizuri kwa kuhakikisha wanaagiza bidhaa zenye viwango na kuzihifadhi katika mazingira salama ili zisiharibike kabla ya kumfikia mtumiaji.
"Serikalini inayoongozwa na Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha miundombi ya usafiri na usafirishaki ikiwemo ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria, bandari kavu ya Fela, reli ya kisasa (SGR) hadi jijini Mwanza na uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Mwanza ili kurahisisha shughuli za kibiashara" alisema DC Makilagi.
Katika hatua nyingine, Makilagi alionya kuwa wafanyabishara wanaouza bidhaa zenye viambata sumu wanaliangamiza taifa na wanaenda kinyume na lengo la Serikali ya kuhakikisha afya ya wananchi iko salama akisema tafiti mbalimbali zinazoendelea kufanyika zinaonyesha magonjwa kama kansa yanasabanishwa na ulaji wa vyakula pamoja na utumiaji wa vipodozi vyenye viambata sumu.
Pia Makilagi aliipongeza TBS kwa kuendelea kutoa elimu na semina kwa wadau mbalimbali ili kutambua bidhaa zenye ubora na zile zenye viambata sumu zilizopigwa marufuku akisema kila mdau anapaswa kutimiza wajibu ili jamii iwe salama.
Naye Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Mhandisi Joseph Mwaipaja alisema Shirika hilo litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa wafanyabishara wanaoingiza sokoni bidhaa zilizopigwa marufuku ingawa kabla ya kuchukua hatua hizo TBS inawaelimishwa kwanza.
Kwa upande wake mmoja wa wafanyabiashara walioshiriki mafunzo hayo, Mohamed Muhran alisema watazingatia elimu waliyoipata kwenye semina hiyo ikiwemo kuagiza na kuuza bidhaa zilizosajiliwa kusajiliwa kisheria ili kwa pamoja kwa kushirikiana na TBS wafanikishe jitihada za kuondoa sokoni bidhaa zenye viambata sumu.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi akifungua semina hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa TMDA Buzuruga jijini Mwanza.
Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Amina Makilagi (katikati) akifungua semina elekezi ya kuwajengea uelewa wafanyabiashara jijini Mwanza ili kufanya biashara zao kwa kuzingatia sheria hususani kutoingiza sokoni bidhaa zenye viambata sumu. Wengine ni Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Mhandisi Joseph Mwaipaja (kulia) na mwakilishi wa wafanyabiashara Mohamed Muhran (kushoto).
Semina hiyo ya siku moja inatarajiwa kuleta tisha kwa wafanyabiashara ikiwemo kutoagiza na kuuza bidhaa za chakula na vipodozi zilizopigwa marufuku ambapo hatua hiyo ni mwendelezo wa TBS kutoa semina na mfunzo kwa wadau mbalimbali nchini.
Social Plugin