Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionesha vifaa vilivyohujumiwa kutoka kwenye miundombinu ya shirika la umeme Tanzania (Tanesco)
Na Kareny Masasy,Kahama
JESHI la polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu 13 kwa tuhuma ya kuhujumu miundombinu ya nishati ya umeme yenye thamani ya zaidi ya sh Milioni 10 kutoka shirika la umeme nchini (Tanesco) wilayani Kahama.
Walioshikiliwa majina yao yamehifadhiwa ni wananchi wa kawaida saba wakiwemo viongozi wa dini,watumishi wa shirila la umeme Tanesco wawili na vishoka wanne .
Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi ameeleza leo waandishi wa habari tarehe 30/09/2022 kuwa mnamo tarehe 25/09/2022 na tarehe 29/09/2022 polisi kwa kushirikiana na maafisa kutoka Tanesco liliendesha oparesheni maalum iliyolenga kufichua vitendo vya kihalifu vinavyohusisha uhujumu wa miundombinu.
Kamanda Magomi amesema kuwa jumla ya Transfoma 73 za Tanesco wilayani Kahama zimehujumiwa kwa kukatwa wire wa earth rod na kuibiwa earth rod zenyewe hivyo kuhatarisha usalama wa miundombinu hiyo.
“Vitendo hivi ni kinyume cha sheria na vinalikosesha shirika mapato,watuhumiwa ambao ni watumishi wa shirika hilo walikuwa wakishirikiana na vishoka kufanya vitendo vya kuhujumu miundombinu ya shirika kwa kuiba vifaa na kuwaunganishia wateja bila kufuata utaratibu”amesema Kamanda Magomi.
Kamanda Magomi amesema upelelezi unaendelea na wakibainika watafikishwa mahakamai na kutoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa Shinyanga kuacha tabia hiyo mara moja na yeyote atakaye bainika atachukuliwa hatua za kisheria
Kaimu Meneja wa Tanesco wilaya ya Kahama Mhandisi Tumaini Chonya amesema kuwa watuhumiwa hao wameiba boksi na kuunganishia nyaya ambapo wanatumia bila kulipia umeme lakini pia ni hatari kwa sababu inakuwa haina earth rod wakati wa masika kipindi cha mvua radi ikija inaweza kuunguza nyumba na kusababisha hasara kwa mtumiaji huyo na shirika pia.
“Baadhi ya watumishi wetu wenyewe ndiyo wanafanya mchezo huo lengo lao ni kutumia tu bila kulipia muda wote na wewe mwananchi ukiona hivyo kwanini usishtuke hujuma hiyo inaongeza gharama kwenye shirika kurudishia miundombinu hiyo sasa haikubaliki wananchi mshtuke unatumiaje umeme wa luku bila kuisha muda wote?”amesema Chonja.
Kaimu meneja kutoka shirika la umeme Tanzania( Tanesco) wilayani Kahama Mhandisi Tumaini Chonya akiangalia vifaa kutoka shirika hilo.
Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akiangalia nyaya za umeme zilizohujumiwa pamoja na rimoti za luku.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi akionesha vifaa.
Vifaa vilivyodaiwa kuhujumiwa kutoka Tanesco.
Social Plugin