Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BARABARA ZA TARURA ZALETA SHANGWE HAI WANANCHI WAMPONGEZA RAIS SAMIA



Ujenzi wa barabara za Makoa Darajani-Mferejini (7.3 KM) na Kwasadala -Longoi (6.0 KM) kwa kiwango cha changalawe umeleta faraja na furaha kubwa kwa wananchi wa kata ya Narumu na maeneo mengine ya jirani wilayani Hai, Kilimanjaro kwa kuwaondolea kero kubwa ya barabara iliyodumu kwa muda mrefu.


Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa barabara hizo mbele ya Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Babara Vijijini na Mijini (TARURA) meneja wa TARURA wilaya ya Hai mhandisi Pickson Lema alisema ujenzi wa barabara hizo uliogharimu shilingi 950,000,000.00 utawawezesha wananchi kuzifikia huduma muhimu za kijamii kama shule, hospitali, nyumba za ibada na masoko kiurahisi.

Alibainisha pia barabara hizo zitawezesha usafirishaji wa mazao ya chakula na biashara kiurahisi.

Diwani wa Kata ya Narumu Mhe John Lengai alisema kuwa anamshukuru Rais Smia Suluhu Hassan kwa mambo mazuri anayoyatekeleza na mojawapo likiwa ni hilo la barabara ukiachilia mbali vituo vya afya, zahanati na madarasa anayojenga, akamwomba mwenyekiti wa bodi kufikisha salamu hizo kwa Rais kwa kuwatendea makuu.

Kwa upande wake katibu wa mbunge wa Hai ndugu Benson Lema alisema kuwa anatoa shukurani za dhati kwa bodi ya ushauri ya TARURA pamoja na TARURA mkoa na wilaya kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja.

“Lakini shukurani za dhati ziende kwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan. Kwakweli ametupendelea kwa upekee kabisa kwani barabara hii kutokana na ubovu wake ilikuwa inaitwa barabara ya Ngómbe lakini sasa na sisi tunaonekana watu kwa barabara safi kabisa,” alisema Benson

Marry Shirima mtendaji wa kata ya Narumu alisema kuwa kwa niamba ya mbunge na wananchi wa kata yake wanamshukuru sana Rais Samia suluhu Hassan pamoja na TARURA kwa barabara hizo zinazojengwa.

“Mimi ni mtendaji wa kata hii na ninaposafiri ukinikuta utafikiri nimetoka kuvuna kumbe ni kwasababu nimepita kwenye maeneo magumu ambapo kulikuwa hakuna usafiri unaweza kufika kwenye hili eneo, lakini kwa sasa bodaboda zipo za kutosha na magari yatakuwa yakutosha pia,”alisema Marry.

Aidha alimkabizi mwenyekiti wa bodi kahawa pamoja na mkungu wa ndizi kama ishara ya ukarimu na moyo wa upendo kutoka kwa wananchi kwa barabara nzuri walizojenga.

Mwenyekiti wa bodi ya Ushauri ya TARURA mhandisi Florian Kabaka kwa upande wake alisema kuwa wamefika wilayani hapo kwa lengo la kukagua barabara ili kuona kama imejengwa kwa ufanisi badala ya kukaa ofisini na kuangalia kwenye makaratasi.

“Ninashukuru kuona kwamba kuna kitu kizuri kinatekelezwa hapa kutokana na furaha na shangwe mliyoionesha hapa, nia njema ya Rais wetu ni kuona tunawafikia wananchi ili wapate miundombinu bora itakayowawezesha kuzifikia huduma muhimu na maeneo ya biashara na kukuza uchumi wao,” alisema mhandisi Kabaka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com