TARURA YAONDOA KERO YA WANANCHI SAME KWA KUFUNGUA BARABARA MPYA


Ujenzi wa barabara mpya ya Mpirani Dispensari – Dindimo Primary School (4.30 KM) inayojengwa kwa kiwango cha changarawe katika kata ya Bombo Wilaya ya Same utawapunguzia wananchi kero ya kutembea kwa takribani kilomita 18 wakitumia barabara ya mzunguko ya Maore – Vuje – Bombo.


Akizungumza mbele ya bodi ya ushauri ya TARURA iliyofanya ziara ya ukaguzi, kaimu meneja wa TARURA Wilaya ya Same mhandisi James Nyamega alisema barabara hiyo itakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa kata ya Bombo na Maore kwasababu ni fupi.

“Barabara hii mpya itarahisisha wananchi kwenda kupata mahitaji maeneo mbalimbali, sambamba na usafirishaji wa mazao hasa Tangawizi ambayo inalimwa kwa wingi maeneo ya milimani,” alisema James.

Diwani wa kata ya Maore Mhe. Rashid Juma alisema kuwa wameipokea barabara hiyo kwa furaha sana kwani imeongeza mahusiano ya ujirani mwema kati ya bombo na maore kwani mwanzo walikuwa wakitumia nauli ya shilingi 14,000 lakini sasa kwa barabara mpya nauli itakuwa 7,000 hivyo kurahisisha usafiri na usafirishaji.

“Sisi wana Maore tunasema kwamba tunashukuru sana TARURA na Serikali kwa ujumla kwani imetusaidia sana sasa itakuwa rahisi kutoa mazao kutoka milimani kwenda masokoni,” alisema Juma.

Aidha Mhe. James aliomba ufafanuzi kwa viongozi wa TARURA kuhusu mtu mmoja aliyedai kuwa yeye ndiye aliwatafuta wafadhili kwa ajili ya kutengeneza barabara hiyo ili wananchi wawe na ufahamu.

Akijibu hoja hiyo mtendaji mkuu wa TARURA mhandisi Victor Seff alisema anashangaa hoja hiyo imetoka wapi na yeye kama mtendaji mkuu alitegemea aambiwe kama kuna changamoto yoyote katika ujenzi ili itatuliwe.

“Kama mmesikiliza taarifa ya meneja hapa, hizi pesa ni za Serikali na zimetolewa na Mheshimwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa hiyo hao labda ni watu wanapiga porojo tu. Hii pesa inatoka Serikalini na ndiyo maana tumekuja kukagua kama pesa imetumika ipasavyo au labda kama barabara imejengwa chiuni ya kiwango ili tuchukue hatua hapahapa lakini naona hilo halipo,” alisema Seff.

Angela Mgonja mkazi mkazi wa Kijiji cha Mpirani, alisema kuwa wanamshukuru sana Mungu kwa barabara hiyo kwani walikuwa wakiamka saa nane za usiku kuanza safari ya kwenda Maore sokoni wakiwa na vitochi tu.

“Lakini kwa sasa hivi tunamshukuru Mungu sana kwa ajili ya maendeleo yetu na kwa ajili ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan, Mungu ambariki,” alisema Angela.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post