SERIKALI YAFUTA TOZO..HUU HAPA UFAFANUZI



Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba
 **

Hatimaye Serikali imesikia kilio cha Watanzania kwa kufuta na kupunguza kiwango cha tozo za miamala ya kieletroniki.

Uamuzi huo umetangazwa leo Jumanne Septemba 20, 2022 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba bungeni baada ya kipindi cha maswali na majibu.

Amesema Serikali imepunguza wigo wa tozo, kuchochea matumizi ya miamala kwa ajili ya kupunguza fedha taslimu, kurahisisha utozaji na kuzuia kutoza tozo husika mara mbili.

“Marekebisho yaliyofanyika ni kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote) na kufuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote),”
amesema.
👇👇

          KAULI YA SERIKALI KUHUSU TOZO IKITOLEWA NA MHESHIMIWA DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU (MB),

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO

______________________________

 

Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa, katika mwaka wa fedha 2021/22, Sheria ya Malipo ya Taifa, Sura na. 437 (National Payment System Act, Cap. 437) ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2021 na kuanzisha tozo ya miamala ya kutuma na kutoa fedha kwa njia ya simu za mikononi yaani, Mobile Money Transaction Levy. Sambamba na tozo hii, tulipandisha tozo kwenye mafuta kwa ajili ya kutunisha mfuko wa TARURA na Mfuko wa Elimu ya juu. Lengo la kuanzisha tozo hizi ni kuunganisha nguvu na umoja wa Watanzania wote katika kuiwezesha Serikali kuongeza kasi ya kutekeleza miradi hasa ile iliyokosa fedha kutokana na ufinyu wa bajeti ili kuwakwamua wananchi dhidi ya ukosefu wa huduma za jamii-msingi kwa kuzingatia kuwa sura ya bejeti yetu karibu kila mahitaji ni mahitaji ya lazima.Mahitaji ya lazima yanayolindwa kwa mfano SGR, TANROADS, Bwawa la Umeme, REA, TARURA, Maji, Elimu, Mikopo ya Elimu ya Juu, Elimu bila Ada, Mishahara, Deni la Taifa, Afya ni takribani 27.9 trilion na makusanyo ya ndani ni takribani 28.01trilioni.

 

Mheshimiwa Spika, Serikali haina malengo ya kutoza Wananchi wake kodi/tozo kwa ajili ya kuwapa mzigo tu, bali inalenga kuwahusisha Watanzania wote kwa umoja wetu katika juhudi za kujikwamua kimaendeleo.  Kwa mfano, tulipofanya uamuzi huu:  

 

a)   Tulikuwa na hali mbaya sana ya barabara za vijijini zilizokosa matengenezo kwa ufinyu wa bajeti, kadhalika, tulikuwa na vijiji ambavyo havijawahi kuwa na barabara ya aina yeyote tangu nchi hii ipate uhuru, akina mama wajawazito walikuwa wakibebwa kwa vitanda kupelekwa hospitali na wengine kupoteza maisha njiani, watoto wa shule wakibebwa na maji kwa vijito tu kukosekana kwa madaraja;

 

b)   Tulikuwa na kilio kikubwa sana cha ukosefu wa vituo vya afya vya kisasa vijijini, wagonjwa wote walikuwa wanalazimika kutegemea hospitali za wilaya tu, maeneno mengine hata hospitali za wilaya hazikuwepo, sehemu nyingine wananchi walilazimika kwenda hospitali za mikoa jirani. Tulikuwa tunapoteza maisha ya watanzania kutokana na umbali wa kufuata huduma za afya;

 

c)   Tulikuwa na kilio kikubwa cha uwepo wa maboma ya madarasa na nyumba za walimu yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi na yaliyokaa muda mrefu bila kukamilishwa  ilhali kukiwa na uhitaji mkubwa wa madarasa kutokana na ongezeko kubwa la watoto;

 

d)   Tulikuwa na kilio kikubwa cha wanafunzi waliokosa mikopo ya elimu ya juu wapatao 26,000 wakijumuisha mwaka juzi na mwaka jana. Hawa ni watoto wa kitanzania hasa hasa wanaotoka katika familia masikini ambao ndoto zao za kufika chuo kikuu zilikuwa zinaishia hapo; na

 

e)   Tulikuwa na kilio kikubwa cha maji hasa hasa vijijini, jambo hili lilikuwa linaathiri sana shughuli za maendeleo kwa mfano kila mtoto abebe galoni ya maji na kuibajeti kwa siku nzima, walimu kufuata maji maeneo ya mbali, vijana wanaotaka kujenga kuingia gharama kubwa kwa kununua maji yanayopimwa kwa ndoo pamoja na kukosekana kwa mahitaji ya maji katika maeneo muhimu kama Hosipitalini.

 

Mheshimiwa Spika, makusanyo ya tozo ya miamala yameiwezesha Serikali kutoa huduma za msingi za Wananchi wetu katika mwaka wa fedha 2021/22. Mathalani, Serikali ilitumia jumla shilingi bilioni 7 zilitokana na tozo ya miamala kwa ajili kujenga madarasa. Vilevile, Serikali ilitumia jumla ya shilingi bilioni 143.7 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 117 sawa na asilimia 81.4 ya fedha zote zilitokana na tozo ya miamala. Kadhalika, Serikali ilitumia jumla ya shilingi bilioni 611.3 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 221.3 zilitokana na tozo. Kwa upande wa TARURA, Serikali ilitumia jumla ya shilingi bilioni 735.7 kwa ajili ya ujenzi wa barabara vijijini ambapo kati ya kiasi hicho shilingi bilioni 13.5 zilitokana na tozo kwenye miamala na kiasi kingine ni tozo kwenye mafuta.

 

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/23, kulikuwa na mahitaji muhimu na ya lazima ambayo yangekosa fedha kutokana na ufinyu wa bajeti. Baadhi ya masuala muhimu ambayo yangeathiriwa kama tungefuta kabisa chanzo hiki ni:

 

a)   Tungeelekeza fedha za mkopo wa ECF kwenye madarasa mwaka huu, tusingeweza kupeleka bilioni 954 kwenye kilimo zinazolenga kujenga miundombinu ya umwagiliaji, mbegu bora pamoja na block farming. Serikali ilitumia busara ya kiuchumi kupeleka fedha hizo kwenye sekta za uzalishaji ili kutengeneza ajira kwa vijana, na fedha za kutoa huduma za jamii zitafutwe kutoka kwenye tozo;

 

b)   Tungeelekeza fedha za mkopo wa ECF kwenye ujenzi wa VETA mwaka huu, tusingeweza kupeleka bilioni 145 kwenye mifugo, uvuvi na wamachinga zinazolenga kujenga na kununua boti za uvuvi, kuchochea ukuaji wa sekta ya mifugo na kujenga miundombinu na mitaji kwa wamachinga. Katika suala hili pia, Serikali ilitumia busara ya kiuchumi kupeleka fedha hizo kwenye sekta za uzalishaji  na fedha za kutoa huduma za jamii zitafutwe kutoka kwenye tozo;

 

c)   Tungeelekeza fedha za mkopo wa AfDB kwenye ujenzi wa madarasa na VETA mwaka huu, tusingeweza kupeleka bilioni 150 kwenye ruzuku ya mbolea ili kuwasaidia wakulima wazalishe chakula cha kutosha kwa ajili ya nchi yetu na kudhibiti mfumuko wa bei. Hapa pia, Serikali ilitumia busara ya kiuchumi kupeleka fedha hizo kwenye sekta za uzalishaji  na fedha za kutoa huduma za jamii zitafutwe kutoka kwenye tozo; na

 

d)   Tungeamua kutotoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kwenye mafuta kila mwezi tungeweza kuelekeza fedha hizo kujenga madarasa yote, VETA na mengineyo. Hata hivyo, tungeweza kuwa na mfumuko wa bei ambao ungeleta athari kubwa kwenye uchumi ikiwemo kupanda kwa gharama za maisha ambazo zisingehimilika hususan kwa wananchi wa kawaida.

 

 

Mheshimiwa Spika, Hivyo, Serikali ilitarajia kukusanya takriban shilingi bilioni 500 kutokana na tozo ya miamala ya simu na benki na kuzielekeza katika;

 

a)   Ujenzi wa madarasa 8,000 nchi nzima ambapo mahitaji ya madarasa bado yanakadiriwa kuwa 17,000;

 

b)   Kujenga vyuo vya VETA 72 kwenye Wilaya zisizo na vyuo vya ufundi nchini;

 

c)   Kutekeleza mpango wa elimu bila ada kwa kidato cha tano na sita; na

 

d)    Kuendelea na ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na vifaa tiba katika maeneo ambayo bado hayana huduma hizo. Nawasihi Watanzania wote kuunga mkono juhudi hizi njema za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu, Samia Suluhu Hassan.

 

Marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022

 

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2021 ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Malipo ya Taifa, Sura ya 437 (The National Payment System Act, Cap 437) kwa kuanzisha tozo ya miamala ya kutuma na kutoa fedha ambapo Kanuni ya Sheria husika (The National Payment System (Electronic Money Transaction Levy Regulations 2021)) ilianzishwa na kuainisha  tozo kwenye miamala ya kielektroniki ya kutuma na kutoa fedha kwa njia ya simu. Vilevile, kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022, Kanuni za Malipo ya Taifa (The National Payment System (Electronic Money Transaction Levy) Regulations 2021) zilifanyiwa marekebisho kwa lengo la kuongeza wigo wa tozo hiyo kwa miamala yote ya kielektroniki. Marekebisho hayo yalihusisha miamala ifuatayo ya kielektroniki ambayo inalalamikiwa;

 

a)   Kuhamisha fedha kutoka akaunti ya Benki ya mtumiaji kwenda mitandao  ya simu;

 

b)   Kuhamisha fedha kutoka akaunti ya Benki ya mtumiaji kwenda akaunti nyingine ya mtumiaji  ndani ya  benki husika;

 

c)   Kuhamisha fedha kutoka akaunti ya benki ya mtumiaji kwenda akaunti ya benki nyingine;

 

d)   Uhamishaji wa Fedha kimataifa;

 

e)   Kutoa fedha taslimu kutoka akaunti ya simu ya mtumiaji au akaunti ya benki kwa mkusanyaji, wakala wa mkusanyaji au mashine ya kuhesabu fedha kielektroniki.

 

Mheshimiwa Spika, Kuongezwa kwa wigo wa utozaji wa tozo za miamala kumepelekea malalamiko hasi kutoka kwa wadau. Wapo waliodhania gharama zote hizo zimeletwa na Serikali ili hali gharama za kutuma au kutoa fedha zimejumuisha gharama za taasisi husika na nyongeza kidogo ya Serikali. Kwa mfano unapotoa TZS 15,000 ni TZS 2,443, Gharama ya Benki ya Tangu zamani ni TZS 2,200 na tozo ya Serikali yaani gharama mpya ni TZS 243, na kwenye kutuma zaidi ya milioni tatu  kielektoniki (T.T) gharama ilikuwa TZS 14,000 ambapo gharama za Mabenki tangu zamani ni TZS 10,000 na tozo ya Serikali ni TZS 4,000.

 

Mheshimiwa Spika, Kufuatia malalamiko hayo, Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kiliielekeza Serikali kupitia upya tozo za miamala na kuzingatia maoni ya wananchi. Wizara ya Fedha na Mipango kupitia wataalam wake wa Bajeti na wataalam wa Sera wakiwashirikisha wadau wamefanyia kazi maelekezo ya Chama na Maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia upya tozo hizo.

 

Mheshimiwa Spika, naomba kusisitiza hapa wataalam wa Wizara ya Fedha na Mipango wanaohusika na maswala ya Bajeti na Sera wamefanya mapitio haya wakiwa Ofisini kama Sehemu ya Majukumu yao ya Kila siku tofauti na taarifa zilizozungushwa kuwa kuna tume ya watu 200 imeundwa na inatumia mabilioni ya fedha. Napenda kuwasilisha taarifa kuwa tumefanya mapitio kama ifuatavyo:  Kupunguza mzigo wa tozo kwa jamii, Kuchochea matumizi ya miamala kwa njia ya fedha taslimu (cash); Kurahisisha utozaji, na Kuzuia utozaji wa tozo husika mara mbili kwa kuwa utozaji wake kwa sasa unahusisha pande zote mbili yaani mtoaji na mpokeaji.

 

Marekebisho Yatakayofanyika

 

Mheshimiwa Spika, marekebisho yatakayofanyika ni kama ifuatavyo;

 

a)   Kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote);

 

b)   Kufuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote);

 

c)   Kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine (pande zote);

 

d)   Wafanyabiashara (merchants) hawatahusishwa kama ilivyo kwenye kanuni za sasa;

 

e)   Kusamehe tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki na ATM kwa miamala yenye thamani isiyozidi shilingi 30,000; na

 

f)    Kupunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kufuatana na kundi la miamala. Ikumbukwe kuwa tozo hizo ambapo viwango vya tozo vilishushwa kwa asilimia 30 kutoka kiwango cha juu cha shilingi 10,000 hadi kiwango cha juu cha shilingi 7,000, viwango ambavyo vilianza kutumika tarehe 07 Septemba, 2021. Kadhalika, Mheshimiwa Rais alisisitiza kupunguzwa zaidi tozo ambapo Wizara ya Fedha ilipunguza tozo zaidi kwa kushusha tena kiwango cha juu kutoka 7,000 hadi 4,000.

 

Mheshimiwa Spika, marekebisho haya yataanza kutumika tarehe              1 Oktoba 2022.

 

Mheshimiwa Spika, Sambamba na hatua hiyo, Serikali inafuta utaratibu wa kodi ya zuio inayotokana na pango kukusanywa na mpangaji na badala yake jukumu hilo linarejeshwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utaratibu utakao bainishwa kwenye kanuni. Napenda kusisitiza kuwa kodi ya zuio ya pango siyo ya mpangaji bali inapaswa kulipwa na mpangishaji ambaye ndiye anapokea mapato kutokana na uwekezaji au biashara ya kupangisha. Utaratibu huo umekuwa ukitumika kwa muda mrefu kwenye nyumba za biashara na nyumba zinazopangishwa kwenye makampuni au mashirika yanayofunga ritani za kodi.

 

 

 

 

 

 HITIMISHO

 

Mheshimiwa Spika, mwisho lakini sio kwa umhimu nisisitize mambo mawili:

 

1)      Ni dhahiri kwamba punguzo hili litapunguza mapato ya Serikali, naelekeza fedha hizi zifidiwe kutokana na kubana matumizi mengineyo ndani ya Serikali ambayo hayataathiri utekelezaji wa majukumu ya Msingi ya mafungu husika. Namwelekeza Mlipaji Mkuu wa Serikali kukaa na Maafisa Masuuli wote kuyaangalia upya mafungu ya matumizi Mengineyo ili miradi ya maendeleo yote isiathirike kwa hatua hii. Tukate kwenye chai, vitafunwa, misafara kwenye safari za ndani na nje kwa maafisa wa Wizara zetu kama Mhe Rais alivyoelekeza, tukate Mafunzo, Semina, Matamasha, Warsha, makundi yanayokwenda kukagua mradi ule ule kwa nyakati tofauti au makundi yanayokwenda eneo lilelile kila mtu na gari lake (Mfano, Wilaya ile ile kila Afisa na gari peke yake, Mkoa ule ule kila Kiongozi na gari pekee yake).

 

 

Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.

 

 

Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb.)

Waziri wa Fedha na Mipango,

Septemba 20, 2022. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post