Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa 17 inayozalisha pamba hapa nchini, ukiwa katika msimu wake wan ne (4) tangu zao hili litambulishwe rasmi msimu wa 2017-18.
Pamoja na kuwa miongoni mwa mikoa mipya kiuzalishaji kwa jitihada za uongozi wa mkoa Dodoma na kushirikiana na Bodi ya Pamba imefanikiwa kufikisha zao hili katika wilaya zake tatu hadi sasa huku wilaya ya Chemba ikiwa miongoni mwa hizo wilaya nyingine ni Bahi na Chamwino.
Katika kuendelea kuhakikisha kuwa kilimo cha pamba kinasambaa kwa wakulima wengi na kufanyika kwa tija Bodi ya Pamba inahakikisha kuwa haiwaachi nyuma wakulima kwa kuwapa elimu ya Mara kwa Mara juu ya Kanuni Kumi za kilimo Bora cha Pamba. Katika muendelezo wa kampeni ya uongezaji tija kwa kumtumia balozi wa pamba maeneo mbalimbali yamefikiwa hadi sasa.
Wakulima wa zao la pamba wilayani Chemba wametakiwa kulima zao Hilo kwa kutumia Vipimo vipya vya sentimeta 60 kutoka mstari hadi mstari na sentimeta 30 kutoka shimo Hadi shimo na kuachana na mtindo wa zamani wa kurusha mbegu.
Hayo yamebainishwa na Balozi wa Bodi ya Pamba Tanzania Aggrey Mwanri kwa nyakati tofauti tofauti alipokuwa akitoa semina elekezi namna ya kuongeza tija kwa kutumia Vipimo vipya katika zao hilo kwa wakulima wa vijiji vya Kidoka, Ombili, Paranga na Kelema.
Mwanri amesema kuwa Mabadiliko hayo ya vipimo yataweza kumuongezea mkulima idadi ya miche kutoka 22, 222 ya awali alipokuwa anatumia vipimo vya sentimeta 90 kwa sentimeta 40 hadi kufikia miche 44,444 kwa kutumia vipimo vipya.
Amesema kuwa endapo wakulima watatumia Vipimo vipya wakati wa kupanda zao la Pamba ifikapo mwaka 2025 wanatarajia kuzalisha tani zipatazo Mil 1 ambapo watakuwa wa kwanza Afrika katika uzalishaji wa Pamba.
" Kama wakulima wakifata maelekezo na kanuni Bora za kilimo Cha zao la Pamba kwa kupanda shamba zima kwa kutumia Vipimo na kuachana na mtindo wa kupanda mstari wa mbele kwa kufata vipimo alafu wanaendelea kumwaga mbegu Kama zamani hatutafikia malengo tuliyojiwekea", alisema Mwanri.
Amesema kuwa Pamba ni zao muhimu la kimkakati, kibiashara hapa Nchini na linachangia takribani Asilimia 10 hadi 20 ya Pato la Taifa na fedha za kigeni pamoja na kutoa Ajira kwa Asilimia 40 ya watanzania hivyo wakulima hawana budi kulima zao Hilo kwa kufata kanuni bora za kilimo ikiwemo kupambana na wadudu waalibifu kwa kutumia dawa.
Aidha amesema kuwa kutokana na wakulima kuwa na uelewa mdogo juu ya ulimaji wa zao Hilo na elimu ndogo ya matumizi ya dawa za kuuwa viwatilifu wameendelea kuchanganya mazao shambani huku kanununi ikimtaka kutochanganya mazao kitu ambacho kinadhoofisha zao hilo la pamba.
"Tunapoendelea kutoa elimu,tutaendelea kuwaelimisha juu ya matumizi sahihi ya dawa pamoja muda mwafaka wa kupulizia dawa na vifaa maalumu vinavyotumika wakati wa kunyunyuzia dawa hiyo",alisema Mwanri.
Sambamba na hayo amefafanua kuwa bodi ya Pamba tayari imeishachukua hatua mbalimbali namna ya kuwasaidia wakulima kupata dawa itakayowasaidia kupambana na wadudu waalibifu shambani.
"Bahati nzuri taarifa tulizonazo ni kwamba sasa wameishaanza kupata dawa ambayo itadili na funza na chawajani na wadudu wengine",alisema Mwanri.
Kamili Makiya ni Afisa kilimo Wilaya ya Chemba amesema kuwa kutokana na programu ya kuhamasisha kilimo cha zao la Pamba wilaya hiyo imeanza kuwa na matarajio ya kunufaika tofauti na kipindi cha nyuma ambapo zao hilo lilianza kuzorota.
"Kwa mfano ukiangalia takwimu za nyuma jinsi tulivyokuwa tuneendesha kilimo mwaka 2018 -2019 tulifanikiwa kuzalisha tani 111 lakini baada ya miaka hiyo tukaachana na programu ya kuhamasisha Mara kwa Mara uzalishaji ulishuka chini 2019_2020 tulizalisha tani 73 mpaka kufikia 2020_2021 tulipata tani 500 kwa mwaka",alisema Kamili.
Aidha alisema kuwa mbali na uzalishaji wa zao hilo kushuka ujio wa Balozi wa Pamba kuanza kuhamasisha wanategemea ongezeko la uzalishaji kuwa tofauti na kipindi cha nyuma, sambamba na elimu ya kilimo Bora waliyoipata hivyo kila Kaya wataweza kuzalisha angalau hekali 1 ya Pamba ambapo awali walizalisha kilo 150_250 lakini kutokana na elimu waliyoipata wataweza kufikia kilo 800 .
Jumanne Ally ni mmoja wa wenyeviti amefafanua kuwa semina waliyoipata itawasaidia kuhakikisha pamba itakayo kuwa na tija na itakayowaletea mafanikio kuondoka umasikini katika vijiji vyao.
"Tutaendelea kuhamasisha wananchi kulima zao hilo kwa kufata Sheria na kanuni ya Vipimo vipya na kuachana na vya zamani yatupa mbegu",alisema Ally.
John Joseph na Shabani Hassani ni baadhi ya wakulima waliopata elimu elekezi namna ya kuongeza tija kwenye zao la Pamba wamesema kuwa elimu hiyo itawasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya mabadiliko katika zao hilo, na kuiomba bodi ya Pamba kuendelea kutoa elimu namna ya kuendelea kutumia Vipimo vipya ili waweze kuacha na ulimaji usio kuwa na tija.
Social Plugin