Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWONGOZO WA MPANGO KABAMBE WA AFUA ZA USTAWI WA JAMII WAZINDULIWA DODOMA


Mhe. Captain George Mkuchika akikabidhi Tuzo ya Kutambua Mchango wa Shirika la Pact Tanzania katika kukamilisha na kurasimisha Mwongozo wa Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii kwa Bi. Levina Kikoyo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Pact Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mradi wa ACHIEVE.
 ****

Leo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Majaliwa amezindua Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii (CCSWOP).


 CCSWOP ni Mpango Kabambe wa vipaumbele na bajeti za ustawi wa jamii ngazi ya halmashauri. Mpango Kabambe huu unaratibiwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalumu pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI. 

Kupitia mradi wa ACHIEVE unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID); Shirika la Pact Tanzania limekuwa likifanya kazi na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalumu; kukamilisha, kutekeleza, na kurasimisha Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii (CCSWOP).


 Kazi hizi zinajumuisha utengenezaji wa miongozo, kufundisha kamati za mipango ya ustawi wa jamii kwenye halmashauri zinazofikiwa na mradi, kufanya manunuzi ya vitendea kazi, na kuasisi zoezi la kuambatanisha Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii katika mfumo wakielektroniki wa mipango na taarifa za serikali (PlanRep).

Mpango Kabambe wa Utekelezaji wa Afua za Ustawi wa Jamii unatoa muelekeo na mpangilio wa ujumuishaji wa hatua muhimu zinazochukuliwa na serikali, wadau wa maendeleo na wadau wengine wa huduma za ustawi wa jamii ili kuchochea upatikanaji wa huduma bora na stahiki za ustawi wa jamii.


 Pia, unasisitiza ushirikishwaji na matumizi mujarabu ya takwimu za ustawi wa jamii zinazozalishwa katika ngazi ya halmashauri ili kutengeneza mipango ya ustawi wa jamii yenye kuzingatia ushahidi wa kitakwimu. 


“Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii umeunganishwa katika mfumo wakielektroniki wa mipango na taarifa za serikali (PlanRep) wa Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kurahisisha upangaji, upimaji wa mipango na ufuatiliaji wa mipango na bajeti katika ngazi zote za huduma na maamuzi. Ni rai yangu kuona sasa tunakwenda kupanga na kujumuisha bajeti za wadau wote wa huduma za ustawi wa jamii na kufuatilia utekelezaji wa mipango pamoja na bajeti hizo,” alizungumza Mhe. George Huruma Mkuchika, (MB) – Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais – Kazi Maalum wakati akitoa salamu za Waziri Mkuu.


Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Bi. Kate Somvongsiri alisema, "Kwa miaka sita sasa, tumekuwa tukiunga mkono Serikali ya Tanzania katika kutengeneza mpango huu kupitia miradi ya CHSSP uliokuwa ukitekelezwa na Shirika la JSI kwa kipindi cha 2015-2020 na Mradi wa ACHIEVE unaotekelezwa na Shirika La Pact Tanzania kwa kipindi cha 2020-2024. 

Leo tunashuhudia moja ya hatua muhimu sana ambayo ni urasimishaji. Hii inaonesha ari na juhudi za dhahiri kabisa kati ya Serikali ya Tanzania na Marekani katika kujenga mifumo imara na endelevu yenye nia ya kuboresha maisha hasa miongozi wa makundi maalumu kama vile watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kaya zao. Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii utaenda kuongeza tija, na uratibu maridhawa wa huduma za ustawi wa jamii. Vilevile utaongeza ujumuishi wa huduma kwa makundi maalumu na kuchochea mbinu yakinifu katika kukabiliana na majanga kama vile VVU na UKIMWI.”

Kwa kipindi cha toka mwaka 2020, mchakato wa kukamilisha Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii, umegharimu fedha za kitanzania zipatazo Shilingi 920,174,800/=.


 Tathmini tuliyofanya katika Halmashauri ambazo zimeanza kutekeleza Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii zinaoneshana mabadiliko makubwa katika utengaji wa bajeti na hata kujumuisha bajeti za wadau zenye mlengo wa huduma za ustawi wa Jamii. 


Tunatazamia kuona huduma za ustawi wa jamii kwa watoto wanaosihi katika mazingira hatarishi zikishamari na kuendela kuimarika,” alisema Levina Kikoyo Mkurugenzi Mkazi wa Pact Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa wa Mradi wa ACHIEVE.

Mhe. Captain George Mkuchika akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mwongozo wa Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii
Mhe. Captain George Mkuchika akikabidhi nakala ya Mwongozo wa wa Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii kwa Mkurugenzi wa USAID Tanzania, Bi. Kate Somvongsiri
Mhe. Captain George Mkuchika akikabidhi cheti cha Shukrani kwa Bi. Levina Kikoyo, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Pact Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mradi wa ACHIEVE
Mkurugenzi wa USAID Tanzania, Bi. Kate Somvongsiri akuhutubia wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii
Kikundi cha Ngoma za Asili kikitumbuiza wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Mpango Kabambe wa Afua za Ustawi wa Jamii
Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu akihutubia

Picha ya pamoja kati ya meza kuu na wafanyakazi wa USAID Tanzania na Pact Tanzania



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com