Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATOA HUDUMA ZA AFYA, WANACHAMA WACHANGIA KUHATARISHA UHAI WA MFUKO WA NHIF

 

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu

Na Dotto Kwilasa,DODOMA


SERIKALI kupitia Wizara ya Afya nchini imesema inafanya jitihada kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma na wanachama wa Mfuko wa Taifa wa bima ya afya ( NHIF) vinavyolenga kujipatia manufaa kinyume na utaratibu.


Kutokana na hayo imesema ipo katika hatua za mwisho kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo itaweka mazingira kwa kila mtanzania kuwa na bima ya afya ili kuwezesha dhana ya kuchangiana gharama za matibabu hali itakayo saidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi. 


Hayo yameelezwa leo Jijini hapa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu hali ya mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) na kueleza kuwa Serikali haitakubali kuona Mfuko huo unatetereka hivyo kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wananchi wote kuwa na uhakika wa kupata huduma bora za afya.


Amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya wataaluma 65 wamefikishwa katika mabaraza yao kutokana na kukiuka taratibu na miongozo ya taaluma za afya hivyo kuitaka NHIF kuimarisha mikakati yake ya kupambana na vitendo vya udanganyifu pamoja na kuimarisha matumizi ya Mifumo ya TEHAMA.


Hata hivyo Waziri huyo amewatoa hofu wanachama  wa NHIF na wananchi kwa ujumla kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuuimarisha Mfuko huo ili kuwa endelevu na kuwanufaisha wananchi walio wengi zaidi.


Pamoja na kuimarisha huduma za afya,Waziri huyo amekiri kuwa bado kuna changamoto ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya wananchi wenye magonjwa yasiyo ya kuambukizwa ambayo gharama zake ni kubwa hali inayohatarisha uhai na uendelevu wa Mfuko wa NHIF.

 

Vilevile, changamoto nyingine iliyopo ni uwepo wa kundi kubwa la wananchi wanaojiunga na NHIF kwa hiari ambao, takribani asilimia 99 ni wagonjwa hatua inayotokana na kutokuwepo kwa Sheria ya ulazima kwa wananchi kujiunga na Bima ya Afya na kuondokana na kuelemewa kwa mfuko huo kunakotokana na gharama za matibabu  kuongezeka kwa idadi ya wanufaika wenye magonjwa yasiyoambukizwa na gharama zake, hali inayoweza kuathiri uhai na uendelevu wa Mfuko.


"Kama mnakumbuka tarehe 29/08/2022 wakati nikifungua Mkutano wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika kuhusu Ugonjwa wa Kipindupindu jijini Dar es Salaam, niliweka msisitizo wa kuweka nguvu na jitihada katika kuzuia magonjwa badala ya kusubiri kutibu;


Katika muktadha huo nilitoa angalizo kuwa hivi sasa nchini kwetu tunashudia ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo matibabu yake ni gharama kubwa na hivyo kama tutachelewa kuchukua hatua stahiki katika kudhibiti magonjwa hayo, basi kuna hatari pia kwa Mfuko wetu wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuelemewa na gharama za matibabu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanufaika wenye magonjwa yasiyoambukizwa na gharama zake, hali inayoweza kuathiri uhai na uendelevu wa Mfuko,"Amesema.


Kulingana na takwimu zilizopo, amesema gharama za magonjwa yasiyo ya kuambukizwa zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 35.65 mwaka 2016/17 hadi shilingi bilioni 99.09 mwaka 2021/22 na kwamba Gharama za kuhudumia wagonjwa wa saratani wanaopata tiba za mionzi na chemotherapia (chemotherapy services), kupitia Mfuko ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 22.5 mwaka 2021/22,"amesema


Kwa upande wa huduma za matibabu ya figo kwa wanachama wanaopata huduma ya kuchuja damu (hemodialysis services) Waziri Ummy amesema gharama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 9.5 mwaka 2015/16 kufikia shilingi bilioni 35.44 mwaka 2021/22 huku idadi ya wagonjwa  wa figo imeongezeka kutoka 280 mwaka 2014/15 hadi kufikia 2,099 mwaka 2021/22.


"Gharama za matibabu ya moyo kwa wanachama wa Mfuko wanaopata matibabu ya upasuaji wa moyo (minimal and invasive cardiac procedures), ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 0.5 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 4.33 mwaka 2021/22,gharama za vipimo vya CT scan na MRI ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 5.43 mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 10.87 mwaka 2021/22,"amefafanua 


Sambamba na hayo ameeleza kuwa ni wazi hali ya ustahimilivu na uendelevu wa Mfuko ipo mashakani endapo hatua stahiki hazitachukuliwa ambazo ni pamoja na kuimarisha afua za kushughulikia magonjwa yasiyo ya kuambukiza  katika hatua za awali ikiwemo kuyatambua mapema kabla ya kuwa na athari kubwa,kuongeza idadi ya wanachama na kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma za afya.


Ametaja hatua nyingine ni kudhibiti matumizi ya huduma yasiyo na tija,kupunguza gharama za matibabu nchini,kuwa na Mfumo endelevu wa kuhakikisha Mfuko unakuwa na fedha wakati wote kutoka katika vyanzo vyake vya mapato na katika hatua hii tunaishukuru serikali kwa kuwasilisha michango ya watumishi kwa wakati. 


"Niwatoe wasiwasi wadau wa NHIF wakiwemo wanachama, watoa huduma pamoja na watanzania wote kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha kuwa Mfuko huu unakuwa imara, endelevu na stahimilivu kwani kwa sasa, ni moja kati ya mfumo unaotumika katika kuhakikisha huduma za afya zinatolewa nchini,"amesema


Amesema mfuko wa NHIF ndio umekuwa tegemeo la watanzania wengi hususani wa kipato cha chini pia  umekuwa tegemeo la vituo vya kutoa huduma za afya nchini pamoja na kuwa na wanachama asilimia nane (8) tu ya Watanzania wote, vituo vingi vya kutolea huduma vinategemea mapato kutoka katika Mfuko kwa zaidi ya asilimia 70.


"Katika kuhakikisha kuwa maamuzi yote yahusuyo Mfuko huu yanazingatia taratibu na miongozo ya kuendesha chombo hiki, tumefanya tathmini ya uhai na uendelevu wa mfuko kwa mujibu wa sheria na, hivyo tunatambua ni yapi yanapaswa kufanyika ili kuhakikisha mfuko wetu unakuwa endelevu na imara zaidi na matokeo ya awali yanaonesha uendelevu wa Mfuko huu unategemea sana ongezeko la wanachama watakaoandikishwa katika Mfuko huu,"amesema. 


Akizungumza uzoefu kutoka katika nchi nyingine ,Waziri huyo alisema unaonesha kuwa, kadri idadi ya wanachama inavyokuwa kubwa katika Mifuko hii ya bima za afya za umma kama NHIF, ndipo uwezo wake katika kugharamia matibabu unaongezeka na hivyo kuwa stahimilivu na endelevu kwa muda mrefu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com