BODABODA AKATWA SHINGO, APORWA PIKIPIKI BUNDA



Na Adelinus Banenwa - Bunda
Mtu mmoja ambaye ni dereva bodaboda aliyetambulika kwa jina la ISSA SAGUDA (22) mkazi wa Rubana kata ya Balili, Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara amekutwa amepoteza Maisha kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na tumboni maeneo ya shule ya msingi Rubana.



Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia tarehe 29/8/2022.


Mashuhuda wa tukio hilo wakizungumza na radio Mazingira Fm katika eneo la tukio wamesema wanafunzi waliokuwa wanaenda shule ndo waliogundua kuwepo kwa mwili huo.


“Ilikuwa asubuhi kwenye muda wa saa Moja wanafunzi walikuja kutuita kwamba kuna mtu amekatwa shingo amelala karibu na choo tukaamka haraka na tulipofika tukamuangalia alivyovaa mbele kidogo tukaona alama za break ya pikipiki na pembeni kuna damu na funguo za pikipiki ndipo tulipogundua kwamba huyu ni dereva bodaboda”, amesema shuhuda.



Kwa upande wake mwenyekiti wa waendesha pikipiki maalufu (bodaboda) Wilaya ya Bunda Dickson Joseph amesema tayari wamemtambua.




“Ni bodaboda mwenzetu alikuwa anapaki kwenye kituo Cha NM Bunda Mjini nimepigiwa simu asubuhi kwamba mwenzetu amekutwa amepoteza Maisha na pikipiki imeibiwa ndo nimefika hapa”



Dickson ameongeza kuwa suala ulinzi kwa bodaboda juu ya wateja hasa nyakati za usiku wameshaambizana kutokubali kubeba abiria bila wenzao kuwa na taarifa za mteja unayembeba anatoka wapi na anakwenda wapi.





Kwa upande wake Diwani wa kata ya Balili Mhe Thomas Tamka amesema mauaji yaliyotokea katika kata yake yanaumiza sana na hayakubariki amesema yeye kama mwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata ataitisha kikao ili suala la ulinzi shirikishi uanze mara Moja



Baada ya mauji ya kijana Issa Saguda na kuporwa pikipiki katika mtaa wa Rubana Kata ya Balili Halmashauri ya mji wa Bunda, jeshi la Polisi limesema pikipiki hiyo imepatika eneo la Nyamikoma Wilayani Busega Mkoani Simiyu



Akizungumza na Radio Mazingira Fm Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishina Msaidizi wa Polisi Dismas Kisusi amesema pikipiki hiyo yenye namba za usajili MC 499 CDH aina King lion ilikamatwa na walinzi shirikishi usiku wa tarehe 29 Agosti 2022 masaa machache baada ya kutendeka tukio hilo huku mtuhumiwa akifanikiwa kutoroka.



Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka waliohusika na mauaji hayo huku likitoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kukomesha vitendo hivyo.




CHANZO - RADIO MAZINGIRA FM

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post