Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC KAGERA AVITAKA VYOMBO VYA DOLA KUCHUNGUZA KITUO CHA FORODHA MUTUKULA

 

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Albert Chalamila 

Na Mbuke Shilagi Kagera.


Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Albert Chalamila ameagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa watumishi katika kituo cha Forodha cha Mutukula mpaka wa nchi ya Tanzania na Uganda kutokana na kubainika kwa baadhi ya Watumishi wasio waadilifu kushirikiana na raia kughushi nyaraka na kupelekea Serikali kupoteza mapato.


Akizungumza na Watumishi wa Idara zilizopo katika kituo hicho, Mhe. Chalamila ameeleza kuwa iliundwa kamati ya kuchunguza mwenendo wa usafirishaji wa mazao kutoka Tanzania kwenda nchi ya Uganda na kubaini kuwepo kwa baadhi ya watumishi wasio waadilifu, iligundulika baadhi ya watu kuwa na nyaraka feki ambazo zinatumika kugongwa mihuri kwa kushirikiana na maafisa wa kituo hicho cha forodha na wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.


“Kama mmeona taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera siku chache zilizopita kuna baadhi ya watu ambao waligundulika kuwa na nyaraka feki ambazo zinatumika kugongwa mihuri kwa kushirikiana na maafisa wa kituo hiki cha forodha hivyo Serikali kupoteza mapato,” ameeleza Mhe. Chalamila.


Mkuu wa Mkoa amezitaka Mamlaka za watumishi hao kuchukua hatua za haraka za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kuwahamisha katika kituo hicho cha forodha.


Ameeleza kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera alimtaja mtuhumiwa mmoja ambaye si Mtanzania kumiliki mihuri mitatu ya bandia ambapo vyombo vya dola vinaendelea kumfanyia upekuzi na ambaye imebainika kushirikiana na watumishi wa kituo hicho. 


"Mtuhumiwa huyo alikiri kumiliki mihuri bandia ukiwemo mhuri wa Mamlaka ya Mapato Tanzania aliokuwa anautumia kugonga nyaraka za kuvusha mazao aina ya maharage kutoka Tanzania kwenda Uganda nyaraka ambayo ilikamatwa na Afisa wa Mionzi, afisa huyo baada ya kukamata nyaraka hiyo alimpelekea Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kufahamu kwanini Afisa huyo aligonga mhuri huo ili kuruhusu gari kuingia nchini Uganda bila utaratibu wa mihuri mingineyo kama mhuri wa mazao kutogongwa",ameeleza.


"Baada ya kukagua nyaraka hiyo Afisa wa TRA aligundua mhuri uliotumika ni bandia hivyo kumtaka mtuhumiwa huyo kutoa rushwa ili gari iendelee na safari ya kwenda Uganda. Watumishi hao walifanya kazi nzuri, kubaini nyaraka ya kughushi lakini wakaishia kumuomba rushwa mtuhumiwa",amesema.


Pamoja na hao pia wapo mawakala wa fedha ambao wahusika huwatumia kutuma fedha kwa watumishi wa kituo hicho na baadhi ya mawakala wamekiri kufanya vitendo hivyo.


Kufuatia  hali amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa kuchunguza watumishi wa kituo hicho kwa kushirikiana na mawakala hao ili kuona katika mitandao na kubaini mawasiliano yanayofanyika.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Ndg. Toba Nguvila ameeleza kuwa ziara ya kwanza ya Mkuu wa Mkoa alitembelea mpaka wa Mtukula na kuzungumza na watumishi.


 Katika mazungumzo hayo Mkuu wa Mkoa alitoa maelekezo mengi juu ya uadilifu na nidhamu ya Watumishi katika kusimamia shughuli mbalimbali za kibiashara kati ya nchi na nchi. Na msisitizo mkubwa uliwekwa juu ya kumsaidia Rais Samia kwa vitendo kwa kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali na kusimamia kanuni na taratibu zinazoendesha kituo cha forodha zinazingatiwa.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com