WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA) leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma. Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristu (TCMA) Dk.Paul Kisanga,akisoma risali wakati wa Mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA) leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma. Mkurugenzi wa Mtendaji wa shirika la Christian Social Services Commission (CSSC), Peter Maduki ,akitoa neno la shukrani amemhakikishia Waziri Bashungwa kuendelea kufanya kazi na serikali kwa ushirikiano mkubwa wakati wa Mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA) leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma. SEHEMU ya Washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa (hayupo pichani),wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA) leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma. WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Mkutano wa mwaka wa 85 wa Chama cha Madaktari wa Kikristu Tanzania (TCMA) leo Septemba 5,2022 jijini Dodoma.
..............................................
Na Alex Sonna - Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza Wakurugenzi na Waganga Wakuu wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa Mashirika ya kidini yanatoa huduma za Afya ikiwa ni pamoja na Chama Cha Madaktari Wakristo Tanzania wakati wa kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Ametoa maelekezo hayo leo Septemba 5,2022 Jijini Dodoma Wakati akifunga Mkutano wa 85 wa Mwaka wa Chama Cha Madaktari Wakristo Tanzania (TCMA) uliokuwa na Mada kuu inayosema “Maboresho ya Hospitali za Kanisa katika Utoaji wa huduma za Afya na Upatikanaji wa rasilimali fedha endelefu".
Bashungwa amesema ushirikiano na Mawasiliano hafifu ya Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu kwa taasisi za dini unarudisha nyuma maendeleo kwa jamii hivyo amewaagiza kuhakikisha wanaboresha ushirikiano taasisi hizo ili kutoa huduma bora za afya kwa jamii.
Aidha, Bashungwa amemuagiza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ntuli Kapologwe kukaa pamoja na Chama Cha Madaktari Wakristo Tanzania kufanya mapitio ya mikataba ya Serikali kupitia Halmashauri iliyowekwa na Mashirika ya kidini Kwenye huduma za Afya.
Bashungwa amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuwa na mikataba na mashirika ya dini kutoa huduma kwa wananchi ambapo katika mwaka wa fedha 2022/23, hospitali 87 za mashirika ya dini zina mikataba na Halmashauri kwa ajili ya kutoa huduma za Afya kwa Wananchi.
Vile vile, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea na Juhudi za kuboresha huduma za Afya ambapo katika mwaka wa fedha 2020/21 na 2021/22 Serikali imetumia zaidi ya bilioni 383 kujenga Zahanati 564, Vituo vya Afya 304 na Hospitali za wilaya 68.
Pia, ameeleza Serikali imetumia bilioni 103 kwa ajili ya ununuzi wa Vifaa tiba Kwenda Kwenye vituo vya kutoalea huduma za afya kwa mwaka 2021/22, Vivyo hivyo bilioni 69.9 zimepangwa kutumika kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Awali,Rais wa Chama cha Madaktari wa Kikristu (TCMA) Dk.Paul Kisanga, amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kujadili jinsi ya kuendeleza hospitali za taasisi za dini, kuboresha huduma za afya na kukuza ushirikiano kati ya madaktari na watoa huduma pamoja na kubadilishana mawazo kutafuta njia za kutatua matatizo ya utoaji wa huduma.
“Mada kuu ni kila mwaka inachaguliwa mada maalum inayolengwa kwenye shabaha na kwa mwaka huu tumelenga kwenye maboresho ya hospitali za kanisa katika utoaji wa huduma za afya na upatikanaji wa rasiliamli fedha endelevu,”amesema Dk. Kisanga.
Amesema Hospitali nyingi za makanisa zipo katika maeneo ya vijijini ambako ndiko walipo wananchi wengi na watu wenye uwezo mdogo wa kumudu hali ya maisha.
“Tunafahamu Serikali inavyothamini mchango wa kanisa hadi mwanzoni mwa mwaka huu kanisa kwa pamoja limeendesha vituo zaidi ya 900 vya huduma za afya ikiwemo hospitali 105 ikiwemo tano za Rufaa ngazi ya kanda.
Amesema hospitali 12 zikiwa na huduma za rufaa ngazi ya Mkoa na 37 ni zinatumika kama hospitali za wilaya na kuzifanya hospitali teule.
Amesema wana vituo vya afya 134 kati ya hivyo kuna ambavyo vinalaza wagonjwa wengi kuliko hata hospitali kutokana na mahitaji makubwa.
Amesema wanaipongeza Serikali na Tamisemi kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya na wanauhakika huduma za afya hata zile za kibingwa zitaendelea kuongezeka.
Naye Mkurugenzi wa Mtendaji wa shirika la Christian Social Services Commission (CSSC), Peter Maduki akitoa neno la shukrani alimhakikishia Waziri Bashungwa kuendelea kufanya kazi na serikali.
“Mheshimiwa Waziri nikuhakikishie tupo tayari kufanya kazi na Serikali na kuhakikisha malengo ya serikali ya Raisi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania inafikiwa sisi tunakuhakikishia yote yatafanyika.Na tutakuwa na mikutano kila robo mwaka kwa ajili ya kujadiliana maendeleo na changamoto mbalimbali,” amesema.
Shirika la Christian Social Services Commission (CSSC) linaratibu na kusimamia utolewaji wa huduma za afya kwenye vituo vya afya vipatavyo 900 na huduma za elimu kwenye taasisi za elimu zaidi ya 1000 zinazomilikiwa na taasisi za dini nchini Tanzania.