Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga, limeombwa kufanya uchunguzi wa kina ili kumbaini mtu aliyehusika katika tukio la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka sita, anayesoma darasa la awali katika shule ya Msingi Bugimbagu, iliyopo kijiji cha Bugimbagu, kata ya Mwawaza katika Manispaa ya Shinyanga.
Ombi hilo limetolewa na Babu pamoja na Baba mdogo wa mtoto huyo, ambao kwa pamoja wameiomba Serikali kupitia vyombo vyake kuchunguza kwa kina tukio hilo, ili kumbaini mtu aliyehusika na kumchukulia hatua kali za kisheria.
Akielezea zaidi kuhusu tukio hilo, Baba mdogo wa mtoto huyo , amesema baada ya kufika shuleni alikuta mtoto wao akiwa hawezi kutembea huku akitoka damu sehemu zake za siri, na alipouliza kwa Walimu alielezwa kuwa, wamemkuta akiwa amelala katika eneo la choo cha shule baada ya kupewa taarifa na wanafunzi wenzake, ambapo baada ya kumchunguza walibaini kuwa anatoka damu sehemu zake za siri.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Bugimbagu Bi.Mwajuma Kashinje, amesema alipewa taarifa za tukio hilo na walimu wa shule hiyo, ambapo baada ya kufika shuleni hapo, alimkuta mtoto huyo akiwa ameumizwa vibaya sehemu za siri, lakini hakuna aliyefahamu chanzo cha tukio hilo.
Naye Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Bugimbagu Bi.Neema Ngongi, amekiri kutokea kwa tukio hilo shuleni kwake na kubainisha kuwa, walimkuta mtoto huyo akiwa hawezi kutembea katika eneo la choo cha shule, baada ya kupewa taarifa na Wanafunzi wenzake, ambapo alitoa taarifa kwa mamlaka za juu za shule ikiwemo kamati ya shule na uongozi wa Kijiji, kwa ajili ya hatua zaidi.
Baada ya Redio Faraja kufika katika Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga alipokuwa amelazwa mtoto huyo kwa matibabu, imekutana na Mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt.Luzila John ambaye amebainisha kuwa, walimpokea mtoto huyo hospitalini hapo mnamo Septemba 15, 2022 na kumwanzishia matibabu na kwamba, vipimo vinaonesha aliingiliwa katika sehemu zake za siri na kupata majeraha, ingawa hakutaja moja kwa moja kama amebakwa.
Dkt.Luzila amebainisha kuwa, kwa sasa mtoto huyo ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya hali yake kuendelea vizuri, lakini wanaendelea kusubiri vipimo vingine ambavyo wamevipeleka kwa mkemia mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi.
CHANZO RADIO FARAJA