Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UJENZI WA MADARAJA YA MAWE KUWANUFAISHA WANANCHI HAI


Ujenzi wa madaraja ya upinde wa mawe (stone arch bridges) ya Mkalama–kikavuchini, Ngira na Kisereni unaotekelezwa katika wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro, unatarajiwa kuondoa kero ya muda mrefu waliyokuwa wakiipata wananchi hasa wakati wa kipindi cha mvua na kuwawezesha kufikia huduma muhimu za kijamii.


Wananchi wa kata za Werueru na Masamarundugai wanaounganishwa na daraja hilo walionesha furaha yao kwa wajumbe wa bodi ya TARURA waliotembelea daraja hilo kukagua maendeleo ya ujenzi na kuishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambalo litakuwa na manufaa makubwa kwao.

Akiongea mbele ya wajumbe ya bodi, Mhe. Simbani Waziri diwani wa kata ya Masamarundugai alisema kuwa kabla ya ujenzi wa daraja hilo hali ilikuwa mbaya sana ambapo wananchi walikuwa hawawezi kuvuka wakati wa kipindi cha mvua na shughuli zote zilikuwa zinakwama.

“Kipindi cha masika wanafunzi walikuwa wanalazimika kutembea kwa takribani kilometa 19 kuzunguka ili waweze kwenda shuleni jambo ambalo lilikuwa linahatarisha usalama wao,” alisema Mhe. Waziri.

Naye ndugu Sufiani Mabinga mkazi wa Kijiji cha Kikavuchini alisema kuwa anaishukuru sana Serikali kwa kuwakumbuka kwasababu kwa muda mrefu walitaabika sana na baadhi ya watu walibebwa na maji wakivuka eneo hilo, lakini sasa kero yao itaisha.

“Natoa shukurani zangu za dhati na hasa zimfikie mama Samia Rais wetu, kwa sababu wamepita marais wengi lakini hawajatukumbuka kwa hili, kwa hiyo tunampongeza sana kwa wema wake aliotutendea, “alisema Sufiani.

Shani Halfani mkazi wa Mkalama yeye alisema wanamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Hai mheshimiwa Saashishi pamoja na Serikali nzima kwasababu ya ujenzi wa daraja hilo baada ya kuteseka kwa miaka mingi lakini kwa sasa wanajua wamepata ukombozi.

“Wakati wa mvua wagonjwa walikuwa wanashindwa kupitishwa kwenda hospitali, wakinamama wajawazito wengine wamejifungulia hapa kwenye kivuko, matatizo yalikuwa makubwa sana na ndiyo maana tunamshukuru sana mama Samia kwa kutukomboa,” alisema Shani.

Kwa upande wake ndugu Gilbert Mwoga, mkurugenzi wa miundombinu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI alisema kuwa wakiwa kama watekelezaji wa ilani ya chama tawala, moja ya kipengele katika ilani ni kutumia malighafi zinazopatika katika maeneo ya ujenzi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja hivyo wanaipongeza sana TARURA kwa kutekeleza hilo.

“Daraja hili kwa mujibu wa mhandisi wa Wilaya linagharimu takribani shilingi milioni 200 wakati kama ingejengwa kwa zege lingegharimu takribani shilingi milioni 600, hivyo tumeokoa fedha nyingi ambazo zinaenda kunufaisha maeneo mengine, ni jambo la kupongeza sana, “alisema Gilbert

Mhandisi Florian Kabaka, mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA yeye aliwashukuru wananchi kwa kuonesha furaha yao na kutambua umuhimu wa daraja hilo, hivyo aliwaasa wananchi na viongozi wa eneo hilo kuilinda miundombinu ya daraja hilo ambaya ni kwa manufaa yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com